Atakayebadili matumizi ya fedha za kununua bidhaa za afya kuchukuliwa hatua

NA JAMES MWANAMYOTO
OR-TAMISEMI

NAIBU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Afya) Dkt. Grace Magembe amesema Serikali itachukua hatua dhidi ya viongozi wa Halmashauri watakaobainika kulipa posho za watumishi kwa kutumia fedha ambazo zimetengwa na Serikali kwa ajili ya kununua bidhaa za afya ili kuboresha utoaji huduma za afya msingi nchini.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Afya) Dkt. Grace Magembe (katikati) akiwa katika kikao kazi chao chenye lengo kujadili uboreshaji wa huduma za UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria nchini, kinachofanyika katika Ukumbi wa Ngome Saccos jijini Dar es Salaam.

Dkt. Magembe amesema hayo leo katika Ukumbi wa Ngome Saccos jijini Dar es Salaam, wakati akifungua kikao kazi cha wadau chenye lengo la kujadili uboreshaji wa huduma za UKIMWI, Kifua Kikuu na huduma muunganisho za Afya.

“Nimepita katika halmashauri zenu na kubaini vifungu ambavyo vilikuwa vinalipia bidhaa za afya vimelipia posho, hizo ni hoja za ukaguzi hivyo mtachukuliwa hatua na CAG, Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Wizara ya Afya,” Dkt. Magembe amesisitiza.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Afya) Dkt. Grace Magembe akizungumza na waratibu na wadau (hawapo pichani) wanaohusika na utekelezaji wa afua za UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria wakati akifungua kikao kazi chao chenye lengo kujadili uboreshaji wa huduma za UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria kinachofanyika katika Ukumbi wa Ngome Saccos jijini Dar es Salaam.

Dkt. Magembe amewahimiza washiriki wa kikao kazi hicho kuzingatia miongozo ya matumizi sahihi ya fedha za bidhaa za afya na kuongeza kuwa, kama kiongozi au mtumishi anaona kuna ulazima wa kubadili matumizi ya fedha za bidhaa za afya ni vema akasubiria muda wa kubadili matumizi ya fedha (reallocation) ufike ili mabadiliko yafanyike kwa mujibu wa taratibu.

“Wafamasia wa mikoa, wataalam wa maabara wa mikoa na waratibu wa afya wa mikoa mliopo hapa ni wazi kuwa zoezi la kubadili matumizi ya fedha iwapo kuna ulazima ni jukumu ambalo mnapaswa kulitekeleza wakati wa kipindi cha kubadili matumizi ya fedha (budget reallocation),” Dkt. Magembe amehimiza.
Baadhi ya washiriki wa kikao kazi chenye lengo kujadili uboreshaji wa huduma za UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Afya) Dkt. Grace Magembe (hayupo pichani) alipokuwa akifungua kikao kazi chao kinachofanyika katika Ukumbi wa Ngome Saccos jijini Dar es Salaam.

Sanjari na hilo, Dkt. Magembe amefafanua kuwa, kitendo cha kubadili matumizi ya fedha za afya bila kuzingatia utaratibu kinapekea kuibuka kwa migogoro isiyo ya lazima pindi unapofika wakati wa kulipia bidhaa hizo MSD au kwa mshitiri kwani kifungu husika kinakuwa kimeshatumika kulipia posho au huduma nyingine ambazo haziusiani na bidhaa za afya.
Washiriki wa kikao kazi cha kujadili uboreshaji wa huduma za UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria wakimsikiliza Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Rudifield Peter Mnari (hayupo pichani) wakati akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Afya) Dkt. Grace Magembe kufungua kikao kazi hicho kinachofanyika katika Ukumbi wa Ngome Saccos jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa kikao kazi hicho, Dkt. Kheri Kagya ambaye ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi amemshukuru Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Afya) Dkt. Grace Magembe kwa kuwakumbusha kuzingatia matumizi sahihi ya fedha za bidhaa za afya kwa mujibu miongozo iliyopo na azma ya serikali kutenga fedha hizo ili kuboresha utoaji wa huduma za afya msingi kwa wananchi.

“Kwa niaba ya washiriki wenzangu nina kuhakikishia kuwa tumepokea maelekezo yako na tutayatekeleza kwa vitendo maelekezo yako kwa kuzingatia matumizi sahihi ya fedha za bidhaa za afya,” Dkt. Kagya ameahidi.
Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Luitfrid Nnally akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Afya) Dkt. Grace Magembe (hayupo pichani) kufungua kikao kazi cha wadau chenye lengo la kujadili uboreshaji wa huduma za UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Dawa na Mfamasia Mkuu wa Serikali Bw. Daudi Msasi amesema kuwa kikao kazi hicho ni mahususi kwa ajili ya kujadili umuhimu wa takwimu sahihi katika kufanya maamuzi, ikiwa ni pamoja na kujadili suala la upatikanaji wa bidhaa za afya nchini pasipo kuwa na upungufu utakaoathiri utoaji wa huduma za afya msingi kwa wananchi.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Afya) Dkt. Grace Magembe akichukua dondoo wakati Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Rudifield Peter Mnari (hayupo pichani) akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha kufungua kikao kazi chenye lengo kujadili uboreshaji wa huduma za UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria nchini kinachofanyika katika Ukumbi wa Ngome Saccos jijini Dar es Salaam.

Naye, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Luitfrid Peter Nnally amesema, kikao kazi hicho cha waratibu na wadau wanaohusika na utekelezaji wa afua za UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria kimefanyika kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kubaini changamoto za utoaji huduma za afua hizo pamoja na kuweka mikakati endelevu ya kutoa huduma bora za UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria kwa wananchi.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Afya) Dkt. Grace Magembe akiwa katika picha ya pamoja baadhi ya waratibu na wadau wanaohusika na utekelezaji wa afua za UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria mara baada ya kufungua kikao kazi chenye lengo la kujadili uboreshaji wa huduma za UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria ambacho kinafanyika katika Ukumbi wa Ngome Saccos jijini Dar es Salaam.

Kikao kazi hicho kiliudhuriwa na Makatibu wa Afya wa Mikoa, Waratibu wa Kudhibiti UKIMWI wa Mikoa, Waratibu wa Maabara wa Mikoa, Waratibu wa UKIMWI/TB wa Mikoa, Wafamasia wa Mikoa, Waratibu wa MTUHA Mikoa, Wakurugenzi na watumishi kutoka OR-TAMISEMI na Wizara ya Afya, na kauli mbiu ya kikao kazi hicho ni "Matumizi Bora ya Rasilimali na Takwimu ni Nguzo Muhimu katika Utoaji wa Huduma za Afya nchini."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news