Benki ya Dunia yaipongeza Tanzania mradi wa SGR

DAR-Benki ya Dunia imeshangazwa na hatua kubwa iliyofikiwa na Serikali katika kutekeleza Mradi wa Kimkakati wa Reli ya Kisasa wa SGR, na kuahidi kuwa itaweka mkono wake kusaidia ujenzi wa Reli hiyo muhimu kwa kukuza biashara na ukuaji wa uchumi wa nchi.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam, na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Benki ya Dunia anayesimamia Ujenzi wa Miundombinu, Bi. Wendy Hughes, aliyepo nchini kwa ziara ya kikazi, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mawaziri watatu wa Kisekta, wakiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa na Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. Abdallah Ulega.

Bi. Hughes aliyeambatana na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bw. Nathan Belete na Viongozi wengine waandamizi wa Benki hiyo, alisema kuwa amesafiri kwa kutumia reli hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na kushangazwa na kiwango cha ubora wake wa viwango vya kimataifa.
Alisema kuwa, Benki ya Dunia inaendelea kuchakata maombi yaliyowasilishwa na Serikali katika Benki hiyo, na kwamba iko tayari kusaidia ujenzi wa Reli hiyo ya Kimkakati na kushauri pia sekta binafsi ishirikishwe kikamilifu kuhakikisha kuwa malengo ya kuanzishwa kwa mradi huo yanafikiwa kwa ufanisi mkubwa.

Wakizungumza katika kikao hicho kuhusu Mradi wa SGR, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, na Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Profesa Makame Mbarawa, waliishukuru Benki ya Dunia kwa kuamua kutoa fedha za kujenga mradi huo ambao umefikia hatua mbalimbali za ujenzi na ni mfano barani Afrika na Duniani kwa ujumla

Walieleza kuwa Mradi wa SGR unaogharimu zaidi ya shilingi trilioni 10 za Tanzania, ni muhimu katika kuimarisha biashara na usafirishaji wa abiria na mizigo si tu kwa Tanzania, bali katika nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, ambapo biashara kati ya nchi hizo inatarajiwa kuongezeka na kusaidia kutatua tatizo la ajira kwa wananchi.
Mkutano huo uliowashirikisha Wakuu wa Taasisi katika Sekta ya Usafirishaji na Ujenzi, ulikuwa na ajenda tatu ikiwemo ujenzi wa Mradi wa Mabasi yaendayo haraka Jijini Dar es Salaam-BRT, Mradi wa Reli kwa Kiwango cha Kimataifa-SGR na namna ya kuimarisha ushirikiano katika kutekeleza miradi kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi-PPP.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news