DAR-Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) ameitaka Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) kupitia upya mitaala iliyopo kwa ajili ya uboreshaji wa taaluma inayotolewa na Bodi kwa manufaa ya maendeleo ya Taifa na wananchi wake.
Rai hiyo imetolewa katika ukumbi wa Mikutano wa APC Bunju jijini Dar es Salaam wakati akizindua Bodi mpya ya NBAA itakayofanya kazi kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2024 hadi 2027.
Mhe. Chande alisema kuwa kazi kubwa ya Bodi hiyo ni kusimamia na kukuza tasinia ya uhasibu nchini ili kuhakikisha inatoa mchango stahili katika kukuza Uchumi kupitia huduma za kihasibu na ukaguzi wa hesabu za ndani katika taasisi na mashirika mbalimbali.
Vilevile, Mhe. Chande amesisitiza kufanya kazi kwa uadilifu na uzalendo kwa nchi kwa kuwa nguzo kuu ya Wahasibu na Wakaguzi wa mahesabu ni kufanya kazi bila upendeleo na kwa kushirikiana.
Ameitaka Bodi ya NBAA kuendelea kufanyakazi kwa kuzingatia Sheria, taratibu na Kanuni zilizoiunda Bodi ili kusadifu malengo ya kuanzishwa kwa Bodi hiyo.
Aidha,Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Chande amemshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumteua Mwenyekiti wa Bodi ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) kuanzia Novemba nane mwaka huu.
“Imani yaetu ni kuwa Bodi hii mpya ya NBAA italeta matokeo Chanya ambayo Serikali inayatarajia kwa ujenzi wa Taifa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Kituo cha NBAA Makao Makuu ya nchi Dodoma,”alisema Mhe. Chande.
Alisema kuwa Mhe. Rais ameidhinisha shilingi bilioni 29.8 kati ya shilingi bilioni 30 zilizoombwa na Bodi hiyo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo hicho Dodoma na anaamini watakwenda kujenga ofisi nzuri na ya kisasa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NBAA, CPA, Prof. Sylivia Temu amesema kuwa Mwenyekiti wa Bodi aliyeteuliwa na Mhe. Rais na Wajumbe walioteuliwa na Waziri wa Fedha wanakazi ya kuhakikisha wanachama wake wanazingatia vigezo vya kimataifa katika kuandaa mahesabu ambayo yanatumiwa na wadau mbalimbali.
Pia kuhakikisha Wakaguzi wa Hesabu wanazingatia vigezo vya kimataifa ili kutoa taarifa zinazoaminika kwa wawekezaji ili kuendeleza jitihada chanya za maendeleo ya nchi katika nyanja mbalimbali ikiwemo ya kiuchumi.
"Nchi yetu inakuwa na sasa ipo katika uchumi wa kati wa ngazi ya chini, sisi kama wahasibu tunaungana na juhudi za Serikali katika kutoa taarifa za kihesabu zinazoaminika zitakazo wavutia wawekezaji ili kuondoa mashaka katika suala la uwekezaji.
Prof. Temu amesema kuwa Bodi ya NBAA itatekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Chande kwa kuwa yanachochea utendaji kazi na kuleta ufanisi wenye tija kwa Taifa.