GITEGA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeshiriki katika sherehe za Maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Burundi (BRB) yaliyofanyika tarehe 13 Desemba, 2024.
Katika sherehe hizo, BoT iliwakilishwa na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Yamungu Kayandabila.
Akihutubia katika sherehe hizo, Rais wa Burundi, Mhe. Evariste Ndayishimiye, ameipongeza Benki Kuu ya Burundi kwa mafanikio iliyoyafikia pamoja na changamoto kubwa ilizokumbana nazo katika kipindi chote na hatimaye kufikisha miaka 60.
“Nitoe pongezi kubwa sana kwetu, kwa Gavana wa sasa pamoja na wasaidizi wake, wafanyakazi pamoja na Magavana waliowatangulia, kwa kuifanya Benki Kuu ya Burundi kufanikiwa katika malengo yake pamoja na changamoto lukuki ilizokutana nazo, ikiwa ni pamoja na kupinduliwa kwa serikali mbalimbali ambazo zilikuwa zinaongoza katika vipindi tofauti tofauti,” alisema.Naye Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Kayandabila, aliipongeza Benki hiyo kwa kuweza kufikisha miaka 60 ya utendaji kazi wenye mafanikio.
“Benki Kuu ya Burundi imeonesha ukomavu wa kuendelea kuhudumia taifa la Burundi kwa kipindi chote cha miaka 60 pamoja na kupitia changamoto mbalimbali,” alisema Dkt. Kayandabila katika hotuba ya shukrani aliyoiwasilisha kwa niaba ya Benki Kuu zilizoalikwa, taasisi za kimataifa za fedha pamoja na makampuni mengineyo washirika wa Burundi.
“BRB imekuwa mfano wa kuigwa wa mafanikio na inakuwa ni mfano wa kuigwa na benki kuu nyinginezo, kwani pamoja na changamoto hizo, bado iliendelea kujikita katika majukumu yake ya msingi. Ama kweli Waswahili wanasema, ukimuona nyani mzee porini, basi ujue amekwepa mishale mingi,” alisema Naibu Gavana huyo.
Aidha, akiongea wakati wa kongamano liloandaliwa katika kuadhimisha sherehe hizo, Naibu Gavana wa Kwanza wa BRB, Bi. Irene Kabura, alisema Benki Kuu hiyo ipo katika mchakato wa kuanzisha namna nzuri ya kuwa na Sarafu ya Benki Kuu ya Kidijitali ijulikanayo kama (Central Bank Digital Currency). “BRB bado tunajifunza kutoka kwa benki kuu nyingine ambazo zina hizo fedha za kidijitali za benki kuu punde tutakapojiridhisha, tutachagua njia nzuri za kuendeleza mchakato wa kuwa na fedha yetu ya mtandao ya benki kuu,” alisema.
Pia, maadhimisho hayo yalijumuisha mikutano ya wataalam mbalimbali wa masuala ya uchumi kutoka taasisi mbalimbali za fedha.