BoT yatoa elimu kuhusu Mfumo wa Taarifa za Mikopo kwa watoa huduma ndogo za fedha

MTWARA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaendesha mafunzo kwa watoa huduma ndogo za fedha kuhusu mfumo wa taarifa za mikopo Tanzania.
Lengo la mafunzo hayo ni kuwaelimisha washiriki kuhusu umuhimu wa mfumo huo na kuwahamasisha kuutumia kwa kutoa taarifa za wakopaji wao na kutumia taarifa hizo wanapochakata maombi ya mikopo ya wateja wao.

Mfumo wa taarifa za mikopo ni utaratibu wa kubadilishana taarifa za wakopaji miongoni mwa taasisi zinazotoa huduma za mikopo ili kuleta ufanisi katika sekta ya mikopo.
Semina hiyo, inayofanyika katika Tawi la BoT Mtwara kuanzia tarehe 2 hadi 6 Desemba 2024, inahusisha pia ushiriki wa wawezeshaji kutoka kampuni za ukusanyaji wa taarifa za mikopo nchini, zikiwemo Credit Info na Dun & Bradstreet Tanzania.

Wawezeshaji hao watapata fursa ya kueleza shughuli zao kwa washiriki wa semina, ambao ni wawakilishi kutoka taasisi za huduma ndogo za fedha katika mikoa ya Kanda ya Kusini.

Akitoa mada ya utangulizi, mtaalam kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha BoT, Bw. Gwamaka Charles, ameeleza faida za mfumo huo kuwa ni kuwepo kwa soko la mikopo lenye tija na ufanisi na kuchangia katika kukua kwa sekta ya fedha na uchumi nchini.
“Mfumo huu unapunguza ukosefu wa taarifa kati ya wakopeshaji na wakopaji ili kuwawezesha wakopeshaji kupata historia za waombaji wa mikopo kirahisi na kujenga nidhamu nzuri na uwajibikaji katika soko la mikopo kwa wakopeshaji na wakopaji,” ameeleza Gwamaka.

Ameongeza kuwa mfumo huu unarahisisha upatikanaji wa mikopo kwa wajasiriamali wadogo na wa kati, hivyo kuchochea ajira, vipato, na ustahimilivu wa sekta ya fedha.

“Kuwepo kampuni zinazokusanya taarifa za mikopo, kunapunguza gharama na muda unaotumiwa na wakopeshaji kukusanya taarifa za wateja, na kusaidia kudhibiti athari za mikopo katika taasisi za kifedha ili kupunguza hatari ya kufilisika,”amesema.
Aidha, mfumo wa taarifa za mikopo unasaidia kutumia historia nzuri za mikopo kama mbadala wa dhamana ya mkopo na kupunguza gharama za kukopa (riba na gharama nyingine).

Washiriki wa semina hiyo wanatoka wilaya zote zilizoko katika mikoa ya Mtwara na Lindi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news