BoT:Mabadiliko katika upangaji wa viwango vya riba (coupon rates) za Hati Fungani za Serikali

BENKI Kuu ya Tanzania, ambaye ni wakala wa utekelezaji wa sera ya fedha ya Serikali yaJamhuri ya Muungano wa Tanzania, inapenda kuwataarifu wawekezaji wa Hati Fungani za Serikali na umma kwa ujumla kuhusu mabadiliko katika utaratibu wa kuweka viwango vya riba kuanzia Januari 2025.
Mabadiliko haya muhimu katika kuendeleza masoko ya fedha nchini yanalenga kuhakikisha viwango vya riba za hati fungani vinaendana na hali ya soko wakati wa mnada.

Utaratibu huu unategemewa kuongeza ukwasi katika soko, kurahisisha upatikanaji wa viwango sahihi vya riba na kuongeza ufanisi wa soko la fedha nchini.

Kabla ya mabadiliko haya, viwango vya riba vya hati fungani za Serikali vilipangwa na kubaki bila kubadilika kwa kipindi kirefu na hivyo kutofautiana na riba halisi zinazopatikana katika masoko ya fedha.

Katika utaratibu huu, Benki Kuu itaendelea kuendesha minada ya Hati Fungani za Serikali kama ilivyoainishwa katika Kalenda ya Minada.

Hivyo, kiwango cha riba katika kila mnada wa Hati Fungani kitatangazwa angalau wiki moja kabla ya tarehe ya mnada kwenye tovuti ya Benki Kuu, magazeti na mitandao mbalimbali ya kijamii kupitia tangazo la zabuni (Callfor tender) la mnada husika.

Kutokana na mabadiliko haya, viwango vya riba havitatangazwa kwenye Kalenda ya minada.

Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuwakumbusha wawekezaji kuwa utaratibu wa ushiriki katika minada na uwekezaji wa Hati Fungani za Serikali haujabadilika.

Wawekezaji wataendelea kushiriki kupitia mawakala walioidhinishwa, ikiwa ni pamoja na benki zabiashara na madalali (brokers) wa Soko la Hisa la Dar es Salaam.

Mabadiliko haya hayataathiri Hati Fungani za Serikali zilizotolewa kabla ya Januari 2025.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news