Buriani mwanazuoni na mwanasayansi, Prof.Anselm Biseko Lwoga

NA DEREK MURUSURI
Dodoma

DESEMBA 18,2024 nimeona tangazo la kulala usingizi wa mauti, Prof.Anselm Biseko Lwoga (78), aliyewahi kuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wa pili na Naibu Makamu wa Mkuu Mkuu wa Chuo Kikuu (Taaluma) wa kwanza.
Mwenyezi Mungu amrehemu Prof. Lwoga, ambaye hajaondoka kizembe, la hasha. Ana rekodi ya kipekee sana katika utumishi wake kwa umma wa Watanzania.

Katika uga wa elimu ya juu, hasa katika sayansi, Prof. Anselm Biseko Lwoga ni SHUJAA.

Prof. Anselm Biseko Lwoga ndiye aliyeisuka SUA kufikia mafanikio makubwa ambayo yamepatikana hadi leo.

Ni kwa sababu ya uadilifu, ubunifu, uchapa kazi na maono ya Prof. Lwoga, ambaye pia ni Baba mzazi wa Mkuu wa Chuo cha CBE, Prof. Edda Lwoga. Hakika maji hufuata mkondo.

Ukuaji wa SUA, kwa zaidi ya asilimia 99, unatokana na uongozi mahiri wa Prof. Anselm Biseko Lwoga.

Aliaminiwa na kufanywa Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu (SUA) wa kwanza na miaka minne tu baada ya SUA kuwa Chuo Kikuu kamili.

Akaaminiwa kuwa VC, tena VC wa pili na kukiongoza chuo kikuu hicho kwa miaka 18 hadi tarehe 15 Juni, 2006 alipostaafu.

Alikuwa miongoni mwa viongozi waadilifu sana nchini tena wale wasiopendezwa kabisa na aina yo yote ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma

PROF. LWOGA NDIYO SUA

Ni sahihi kusema kuwa Prof. Anselm Biseko Lwoga ndiye SUA yenyewe.

Kwa miaka 18 kama Mkuu wa Chuo Kikuu, ameacha rekodi kubwa ambayo haitatokea kufikiwa na VC mwingine yeyote, labda Sheria itabadilishwa kurudia matapishi.

Toka tarehe 30 Agosti, 1988, mimi nikiwa kidato cha sita Milambo Sekondari, hadi mwaka nilipokuwa mmoja wa wasaidizi wake kama Meneja wa Biashara na Maendeleo ya Mapato wa SUA, yeye alifanya kazi kwa bidii kubwa hadi kuifanya SUA kuwa Chuo Kikuu chenye heshima kubwa duniani katika fani za Kilimo na Mifugo.

Nikaja SUA. Tukafanya kazi pamoja. Nikajifunza kwake. Nami nikaanza kuandika yale niliyojifunza kutoka kwa Prof. Anselm Biseko Lwoga. Alikuwa hazina kwa Taifa letu na Afrika. Bara la Afrika na mataifa ya dunia yaliitumia hekima na maarifa yake.

SUA ikawa na programu nyingi za Digrii, akavutia fedha nyingi katika utafiti, akasimamia uanzishwaji wa ushirikiano na vyuo vikuu na taasisi nyingi duniani.

Prof. Anselm Biseko Lwoga akawezesha kukua kwa milki ya SUA na akaleta mabadiliko makubwa katika sayansi ya kilimo na ufugaji nchini.

SHAMBA DARASA LA UONGOZI

Kutokana na _mentorship_ yake, uadilifu, unyenyekezi, bidii ya kazi, ustahimilivu, SUA iligeuka kuwa shamba darasa la uongozi.

Viongozi wengi katika Elimu ya Juu waliteuliwa kwa mfululizo kutoka SUA. Hii haikuwa ajali. Kulikuwa na mtu aliyewaandaa watu wake katika medani za uongozi. Na huyu ndiye Prof. Lwoga.

Ni kweli. Si kila mwenye ngozi anaweza kuwa kiongozi. Kuna sifa. Si kila mmojawetu amejaaliwa sifa hizo.

"Prof. Anselm Biseko Lwoga alikuwa kiongozi mnyenyekevu na mwenye kuwatia moyo wengine wafanikiwe," aliniambia Prof. Shaban Athuman Chamshama wa SUA ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Misitu.

ALIWEZAJE KUWA KIONGOZI BORA

Prof. Lwoga alisimamia haki na hakupenda kabisa mapato ya udhalimu.

Aliridhika na kilichokuwa haki yake. Hakuwa kiongozi mwenye tamaa ya kujilimbikizia mali au kupenda makuu. Alikuwa mnyenyekevu lakini mwenye kufuatilia utekelezaji wa mipango iliyopitishwa.

Nilisoma mahali jinsi Wachina walivyo makini na utekelezaji wa mipango yao. Ukiwa kiongozi, mtangulizi wako akaacha mipango yamaendeleo iliyopitishwa, ni lazima uisimamie uliyoikuta na wewe ulete ya kwako.

Dkt. Samia Suluhu Hassan alichokifanya, kutekeleza mipango ya mtangulizi wake, Dkt. John Magufuli na kuleta ya kwake mipya, ndiyo siri ya mafanikio ya China.

Hawaanzi moja kila uchao. Wanaendeleza. Ndio maana wamejenga daraja refu kuliko mengine yote duniani.Daraja linagusa mawingu,imekuwa mnara wa babeli?

Wamarekani wameduwazwa. Ulaya wamechoka kabisa. Wachina wanachanja.

Prof. Anselm Biseko Lwoga alikuwa mwenye maadili ya kupigiwa mfano na mnyenyekevu sana, aliyesisitiza kwenye matokeo.

Ndio maana, baada ya kustaafu, aliendelea kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kuna watu, kutokana na rekodi zisizoridhisha, wakistaafu, hata kwenye warsha hawawezi kualikwa, achilia mbali kuwa Mjumbe au kuaminiwa kuwa Mshauri hata kwenye serikali ya mtaa.

MWENYEKITI WA BODI YA HESLB NA MWANASAYANSI

Mwaka 2009, akiwa mwana sayansi katika mradi uliosimamiwa na Prof. R. B. Mabagala, aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa pili wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Mikopo ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Alihudumu kama Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa HESLB kwa vipindi vyote viwili, 2009-2016.

Kutokana na sifa ya kuheshimu mchango wa kila mfanyakazi na kuhimiza maendeleo, uongozi wake ulishuhudia mageuzi makubwa yaliyolekifanya Chuo Kikuu kuongeza miundombinu ya kujifunzia na kufundishia, iliyopelekea SUA kuongeza udahili kwa kiwango kikubwa.

A TIME WELL SPENT

Siwezi kushangaa kumuona binti yake, Prof. Edda Tandi Lwoga, akifanya mabadiliko makubwa katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).

Prof. Anselm Biseko Lwoga pia ni baba mzazi wa Dkt. Noel Biseko Lwoga, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Makunbusho ya Taifa.

Mafanikio ya uongozi yanaweza kupimwa kwenye _impact_ yako kwa watoto. Mungu alimruzuku karama ya kuongoza si kwa maneno tu bali kwa mfano. Watoto nao wakahamasika. Wakasoma. *"A time very well spent on earth".:

Hakika uongozi si kubeba magunia, ni kutumia bongo. Ni uwezo wa kusimamia maono, maridhiano. 

Ni kuwa Ustahimilivu. Ni kuongoza na kusimamia mageuzi na kuwawezesha watu kusahau yaliyopita na kujenga upya, kuboresha mahusiano na kutazama mbele.

Aliasisi mabadiliko makubwa ya utendaji, yaliyovutia ukuaji mkubwa wa Chuo, ikiwa ni pamoja na kutafuta raslimali fedha zilizosaidia katika ujenzi wa lecture theatres kubwa.

Wazo la kujenga lecture theatres kubwa na nzuri, lilitoka kwake na likatekelezeka kwa ukamilifu, yeye akiwa tayari ameshaondoka kwenye uongozi.

Kuwa mtu mwema ni kupanda mti ambao hutarajii kukaa chini ya kivuli chake. Alianzisha miradi hata akiwa anajua itakamilishwa na wengine.

NILIVYOMFAHAMU KATIKA MIAKA TAKRIBAN MITATU HIVI

Prof. Lwoga hakuwa mtu wa visasi wala majivuno. Alikuwa binadamu aliyejaaliwa ustahimilivu wa hali ya juu na ambaye alikuwa na maneno machache na vitendo zaidi.

Nilibahatika kufanya naye kazi SUA, kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka 2006 alipomaliza kipindi chake cha uongozi na kumwachia Prof. Gerald Monela mwaka 2006.

Prof. Anselm Biseko LWOGA aliyezaliwa katika kisiwa cha Ukerewe mwaka 1946, alisoma shahada zake zote katika Vyuo Vikuu vya Uganda (Makerere), Marekani, Urusi na kufanya kozi mbalimbali katika vyuo vikuu vingi duniani.

Aliwajenga vijana wengi ambao leo ni viongozi. Alikuwa mzalendo, mwadilifu, mstahimilivu, mshauri mzuri na katika miaka 18 kama VC taifa lilitumia ushauri wake katika kufanya maamuzi mengi ya msingi kwani alijaaliwa hekima ya kipekee.

Alimpenda Muumba wake. Prof. Anselm Biseko LWOGA amelala, baada ya kazi kubwa ya kuijenga nchi yetu.

NI HUZUNI SANA

Baada ya kazi kubwa ya kulijenga Taifa letu, Prof. Lwoga amepumzika.

Siku ya Ijumaa (kesho) tarehe 20 Disemba, 2024, mwili wake utapelekwa nyumbani kwake Forest, katika Manispaa ya Morogoro.

Siku ya Jumamosi, tarehe 21 Disemba, 2024, Profesa ANSELM BISEKO LWOGA atalazwa kwa heshima zote katika nyumba yake ya kupumzika, akimsubiria Bwana Yesu katika marejeo yake ya pili hapa duniani.

Hakika amevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo ameumaliza ameimaliza na imani ameilinda (2Timotheo 4:7).

Mwenyezi Mungu amjaaliye usingizi wa amani na pumziko jema hadi tutakapoonana ya pili.

FAMILIA ya SUA, WASUASO duniani kote wanakulilia. Japo ni zamani lakini UDSM pia inakulilia. Watanzania wanakushukuru kwa mchango wako usiofutika. Sasa, ulale kwa amani Baba.

FARE THEE WELL PROFESSOR ANSELM BISEKO LWOGA.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news