DAR-Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam Desemba 15, 2024 lilimpata na kumshikilia,Bwana harusi Vicent Peter Massawe mkazi wa Kigamboni jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu (CDS/IR/2065/2024).
Sambamba na wizi wa kuaminiwa (CDS/IR/2066/2024) baada ya kutengeneza mazingira ya uongo ya kupotea na kutenengeza hisia kwa umma kuwa ametekwa na baadaeye kwenda kujificha Pemba Chakechake Mgogoni kwa mganga wa kienyeji aitwaye Hamis khalid.
Hayo yamebainishwa Desemba 17, 2024 jijini Dar es Salaam na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,SACP Muliro Jumanne Muliro wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Amesema kwamba, ufutiliaji na mahojiano ya kina kati ya Polisi na mtuhumiwa bwana harusi baada ya kupatikana alikiri kutenda makosa hayo ambapo alichua pesa kwa udanganyifu kutoka kwa watu mbalimbali ikiwa ni pamoja Tshs mil.55 na gari namba T 642 EGU aina Toyota Ractis kwa udanganyifu kutoka kwa bwana Sylivester Beda Massawe.
"Alichukua tena pesa Tshs mil. 10 kwa udanganyifu kutoka kwa Ramadhani mkazi wa Magomeni.
"Alichukua pesa pia kwa udanganyifu mil.15 kutoka kwa Ramadhani Bakari mkazi wa Temeke. Mtuhumiwa alichukua pesa pia kwa udanganyifu mil.5 kutoka kwa Resma Mbuguni HR CBE. Alichukua pesa tena mil.4 kutoka kwa Asia Mohamed mkazi Madale.
"Kwa udanganyifu alichukua tena mil.1.5 kutoka kwa Ngoma mkazi wa Kibaha," amesema SACP Muliro na kuongeza,
"Aliendelea tena kwa udanganyifu kuchukua mil.8 kutoka kwa Fauz Suleimani Mussa mkazi wa Tabata baada ya kumuuzia gari ambalo sio lake aliloliazima siku ya harusi yake. Gari namba T642 EGU Ractis mali ya Sylivester Beda Massawe."
Amekumbusha kuwa Novemba 19, 2024 Polisi Kigamboni ilipokea taarifa ya kupotea kwa Vicent Peter Massawe Mfanyabiashara ambaye ilidaiwa hakuonekana tangu Novemba 18, 2024 baada ya harusi yake na alipotea huku akitumia gari Toyota Ractis no T 642 EGU ya Sylvester Masawe ambayo baadaye ilibainika mtuhumiwa aliiuza badala ya kuirudisha kwa mwenyewe baada ya harusi yake Novemba 16, 2024 kwenye ukumbi wa Golden Jubilee.
SACP Muliro amesema, uchunguzi wa mashauri hayo unaendelea na mtuhumiwa atafikishwa katika mamlaka nyingine za kisheria kwa hatua zaidi.
Ametoa wito kwa wananchi kuwa watulivu pindi wapatapo taarifa kuhusiana na matukio ya namna hii na kuviacha vyombo vya kiuchunguzi kufanyia kazi kwa kushirikiana na mamlaka zingine na wananchi.
Aidha, amewaonya na kuwatahadharisha kikundi cha watu wanne ambao amedai kazi yao ni kujenga taharuki kwa umma kuwa kila anayepotea au kutoonekana wao hujitokeza na kuandika kwenye mitandao ya kijamii kuwa watu hao wamechukuliwa na gari hard top nyeupe na kulazimisha hisia kuwa ni vyombo vya dola vimehusika.
Melengo makubwa ya kundi hilo ni kutoa taarifa za uzushi zenye taharuki kwa lengo la kuichonganisha Serikali, Polisi na Wananchi.
Vilevile, Jeshi halitasita kuwachukulia hatua kali na za kisheria wahusika ili kukomesha tabia hizo.