MTWARA-Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe. Abdallah Mwaipaya amewataka Watu wenye Changamoto ya Ulemavu kutobweteka badala yake washiriki katika shughuli zitakazo wakwamua kiuchumi.
Ameyasema hayo Desemba 3, 2024 katika Maadhimisho ya Siku ya watu wenye Ulemavu yaliyofanyika kwenye viwanja vya Zahanati ya Chuno iliyopo kata ya Chuno, Manispaa ya Mtwara-Mikindani.
Akifafanua zaidi alisema kuwa zipo njia mbalimbali za kujikwamua kiuchumi ikiwemo kuunda vikundi vya ujasiliamali na kuomba mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri.
Alisema Serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na watu wenye ulemavu na kuahidi kuendelea kuwashirikiaha kwa kuwapa fursa na nyadhifa mbalimbali zinazojitokeza.
DC Mwaipaya pia alitumia hadhara hiyo kuipongeza Manispaa ya Mtwara-Mikindani kwa kuwawezesha watu wenye ulemavu katika shughuli za maendeleo.
Akizungumza kwa niaba ya watu wenye ulemavu, Abeid Lukanga ametoa rai kwa jamii kuondokana na dhana potofu kuhusu watu wenye ulemavu huku akiomba serikali kuweka miundombinu rafiki katika ofisi zote kurahisisha walemavu kupata huduma kirahisi.
Maadhimisho hayo yaliyobebwa na kauli mbiu ‘Kukuza Uongozi wa Watu Wenye Ulemavu kwa Mustakabaki Jumuishi na Endelevu’ yalianza kwa Mhe. DC kukagua mabanda ya maonesho ya biashara za watu wenye ulemavu na kuunga mkono jitihada zao kwa kununua baadhi ya bidhaa zao.