DCEA na Shirika la Posta Tanzania (TPC) kushirikiana udhibiti wa usafirishaji dawa za kulevya

DAR-Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) na Shirika la Posta Tanzania (TPC) zimetia saini Hati ya Ushirikiano, ikilenga kuimarisha udhibiti wa usafirishaji wa dawa za kulevya, kemikali bashirifu, na dawa tiba zenye asili ya kulevya kupitia mtandao wa posta.
Makubaliano hayo yaliwekwea saini na Kamishna Jenerali wa DCEA, Bw. Aretas James Lyimo, na Postamasta Mkuu wa TPC, Bw. Macrice Daniel Mbodo, ikielezwa kuwa hatua muhimu katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini.

DCEA imebainisha kuwa wahalifu wamekuwa wakitumia mbinu za kusafirisha dawa za kulevya kupitia vifurushi na mizigo. Kati ya dawa zilizokamatwa ni pamoja na mirungi (kilo 39,928.99), heroin (gramu 1,304.17), cocaine (gramu 673.55), na dawa tiba zenye asili ya kulevya kama morphine na codeine.

Ushirikiano huu utahusisha mafunzo ya watumishi, kuboresha vifaa vya utambuzi, na kubadilishana taarifa kwa wakati ili kuimarisha ufanisi wa ukaguzi.
Postamasta Mkuu Bw. Mbodo alisisitiza kwamba Shirika la Posta limejipanga kuhakikisha usalama wa usafirishaji wa bidhaa kupitia mtandao wake. Akirejea sheria na miongozo ya kitaifa na kimataifa, alisema mtandao wa Posta hautaruhusu bidhaa haramu kama dawa za kulevya, silaha, na nyara za serikali kupita bila kugundulika.

Teknolojia ya kisasa imerahisisha usafirishaji wa dawa mpya za kulevya kupitia mifumo ya kifedha ya kidijitali na majukwaa ya siri kama "dark web."

Hata hivyo, mtambo wa kisasa uliotolewa na DCEA umeimarisha uwezo wa TPC kubaini dawa hizo bila kufungua vifurushi, hatua ambayo Bw. Mbodo aliitaja kama nyenzo muhimu ya kukabiliana na changamoto hizi.
Kamishna Jenerali Bw. Lyimo aliwashukuru wadau wote wanaoshiriki katika vita dhidi ya dawa za kulevya, akiwataka Watanzania kutoa taarifa za wahalifu na kushirikiana na serikali kuhakikisha mtandao wa posta unabaki salama. Alieleza kuwa ushirikiano huu unatoa ujumbe wa wazi kwa wahalifu kuwa vitendo vyao havitavumiliwa.

Makubaliano haya yamepongezwa kama juhudi za kuimarisha uchumi na kulinda jamii dhidi ya athari za dawa za kulevya. Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetajwa kuwa mstari wa mbele katika kuwezesha taasisi kama DCEA na TPC kufanikisha mapambano haya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news