ALIYEKUWA Diwani wa Kata ya Bendera wilayani Same mkoani Kilimanjaro kupitia chama cha Chadema mwaka 2015-2020, Michael Mcharo (52), anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa kosa la mauaji ya Edson Shangari (59), mkulima kwa kumpiga risasi tatu mwilini mwake.
Kamanda wa Polisi mkoani Kilimanjaro, SACP Simon Maigwa amesema kuwa, tukio hilo limetokea Disemba 26,2024 majira ya saa tatu na nusu asubuhi huko Kitongoji cha Kaloleni Kijiji cha Bendera katika Kata ya Bendera.
Pia, amedai kuwa, mtuhumiwa huyo alimpiga marehemu risasi tatu, moja mkono wa kushoto, kifuani kushoto na shavu la kushoto ambapo chanzo ni ugomvi baina yao uliotokana na mgogoro wa shamba tangu mwaka 2022.
Kamanda huyo amedai kuwa, mgogoro huo haukupatiwa ufumbuzi hadi tukio lilipotokea juzi.
Amedai kudai kuwa, marehemu alikuwa anaelekea shambani kwake na akiwa njiani hatua chache kabla ya kufika shambani alikutana na mtuhumiwa ambaye alimshambulia kwa kumpiga risasi tatu nakumsababishia kifo.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika kituo cha afya cha Ndungu kusubiria uchunguzi wa Daktari.