DODOMA-Serikali kupitia Wizara ya Madini imefanikiwa kutatua mgogoro uliodumu zaidi ya miaka minne kati ya familia ya Tibe Rwakatare ambao ni wamiliki wa Leseni ya uchimbaji mdogo wa Madini na Juma Kasola ambaye ni mmiliki wa eneo la ardhi lenye ukubwa wa Hekari 9 katika Wilaya ya CHUNYA Mkoa wa Mbeya.
Mgogoro huo umetatuliwa leo Desemba 5,2024 na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa katika kikao cha utatuzi wa mgogoro huo kilichofanyika katika ukumbi wa Abdulkarim Mruma Dodoma baada ya majadiliano na pande zote mbili.
Aidha, katika kikao hicho Tibe Rwakatare alikubaliana na azimio la kurejeshewa ada zote za leseni walizolipia tangu kutolewa kwa leseni husika na Juma Kasola ifikapo Januari 5, 2025 ili aachie eneo hilo lenye ukubwa wa hekari 9 kwa Juma Kasola mara baada ya kurejeshewa gharama hizo.
Sambamba na hayo, Dkt. Kiruswa amezitaka pande zote mbili kuhakikisha zinatekeleza makubaliano hayo na Tume ya madini kusimamia utekelezaji wa mchakato huo kwa mujibu wa sheria ili kulinda haki za pande zote mbili.