Kiini cha Makala
Watanzania ni miongoni mwa wanajamii ya dunia ambao husherehekea sikukuu mbalimbali za dini, mila, utamaduni na za kitaifa.
Shehere hizi huambatana na shamrashara za kufana na kupendeza na miongoni mwa shamrashara hizo huambana na watoto kwenda kwenye matembezi ya kutembelea sehemu mbalimbali za michezo ya watoto zilizopo sehemu mbalimbali nchini katika maeneo ya mijini na vijijini.
Dondoo zifuatazo ni muhimu kuzingatiwa ili kuhakikisha watoto wanasherehekea kwa amani, utulivu, furaha, usalama na kuburudika ipasavyo:
Mosi: Watoto wadogo waambatane na wazazi wao au watu wazima wanaoaminika wanapokwenda kutembea siku za sikukuu. Kamwe watoto wasitoke nyumbani kwenda kutembea wakiwa peke yao.
Pili: Watoto wapewe uongozi na usimamizi ambapo wanatakiwa kuwa sehemu moja na isiwe kila mtoto anakwenda sehemu yake huku msimamizi na yeye akiwa na mambo yake.
Kwa maneno mengine ni wajibu wa mzazi kuwa na umakini mkubwa ili mtoto hata mmoja asichoropoke na kwenda sehemu nyingine.
Tatu: Kuhakikisha watoto wanapata mahitaji wawapo katika matembezi ya sikukuu. Ikiwa mzazi umeamua kuwatoa watoto kwenda kutembea siku ya sikukuu basi hakikisha unabajeti ya shughuli hiyo.
Hii ni kwa sababu watoto hupendelea vitu mbalimbali na wanapokosa na kuwaona wengine wakiwa na vitu mbalimbali ni rahisi kurubuniwa na hata kufanyiwa ukatili wa kijinsia na watu ambao si wema.
Nne: Ni vizuri kuzingatia muda wa kusherehekea na kurudi nyumbani kabla giza halijaingia ili kulinda usalama na maadili kwa watoto.
Nyakati za usiku si nzuri kwa watoto kuwa nje na mazingira ya nyumbani kwenye siku za sikukuu.
Tano: Watoto wadogo wapate vyakula, vinywaji na burudani zote kulingana na umri wao. Kamwe watoto wasipewe pombe ama vileo vya aina yoyote.
Ikiwa mzazi utakosa umakini unaweza kutoa fursa kwa watu wabaya kuwapa watoto pombe, kuwavutisha sigara na hata bangi.
Hitimisho
Dondoo hizi nimezitoa kama sehemu ya kukumbushana tu kwani ninafahamu wazazi wanafahamu vizuri mambo haya.
Hata hivyo, kutokana na wazazi kuwa na shughuli nyingi ni rahisi kujisahau na kuchukua mambo kirahisi na kidhahania kwamba watoto watakuwa salama tu bila usimamizi wowote.
Ni wajibu wa kila mzazi kuzingatia dondoo hizi za Itifaki ya matembezi ya watoto katika siku za sikukuu ili kuhakisha wanakuwa salama, wanapata furaha, hawapotei na hawafanyiwi vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Dondoo hizi nilizotaja ni chache kama sehemu tu ya kukumbusha kama nilivyosema na nyingine wazazi na jamii kwa jumla wanazifahamu.
MWANDISHI
Dkt. Mohamed Omary Maguo
Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Itifaki
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania