MANYARA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Desemba 20, 2024 amekabidhi nyumba 109 kwa waathirika wa maafa ya maporomoko ya tope yaliyotokea Desemba, mwaka jana wilayani Hanang, mkoani Manyara.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi na kuzindua nyumba hizo zilizojengwa katika kitongoji cha Waret, Wilaya ya Hanang, mkoani Manyara, Waziri Mkuu amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anawapa pole waathirika wote na amesisitiza kuwa Serikali itawasaidia ili waendelee na maisha yao kama ilivyokuwa awali.
Amesema kuwa ujenzi wa nyumba 73 kati ya 109 umegharamiwa na Serikali Kuu na kujengwa na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA-JKT); nyumba nyingine 35 zimejengwa na Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania, ilhali nyumba moja imejengwa na Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (UWT).
“Kufuatia maafa hayo, nyumba 109 zilihitaji kujengwa upya kwa haraka. Hivyo, kwa kuzingatia athari hizo, na kwa upendo wake, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia alitoa maelekezo ya kujenga nyumba bora na za kudumu katika eneo salama kwa waathirika waliopoteza makazi yao.
"Ujenzi huu ni ishara ya kujali, upendo na dhamira ya Serikali ya kuendelea kuwa pamoja na wananchi wakati wa shida,” amesema.
Ameongeza kuwa, Rais Dkt. Samia alitoa kiasi cha shilingi bilioni 1.38 kwa ajili ya kuweka huduma za kijamii ikiwemo umeme, maji na barabara za uhakika; lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa kila nyumba inafikiwa na huduma hizo.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang waratibu zoezi la ugawaji wa viwanja vya ziada vilivyopo katika eneo hilo ili kuendeleza eneo hilo.
“Tunataka eneo hili lisitambuliwe kama makazi ya waathirika, bali kijiji rasmi chenye huduma zote muhimu za kijamii na liwe kielelezo cha maboresho ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wote.”
Mapema, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa miongozo, maono na fikra thabiti ya namna ya kukabiliana na kurejesha hali wakati yalipotokea mapororoko ya tope wilayani Hanang.
“Ujenzi wa nyumba hizi ni maono yake, pia ameleta majiko ya gesi 109 ambayo watakabidhiwa wakazi wa eneo hili.”
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha Msalaba Mwekundu, Lucia Sebastian amesema kuwa ujenzi wa nyumba 35 uliofanywa na taasisi hiyo unaashiria umoja ambao unawatambulisha kama Watanzania. “Kwa pamoja, tumetoa makazi; tumetoa amani na usalama kwa familia hizi na tumejenga maisha yao upya. Ushiriki wa TRCS katika safari hii umeongozwa na dhamira yetu ya kusaidia jamii wakati wa shida na dharura,” alisisitiza.
Akizungumza kwa niaba wa wananchi wengine waliokabidhiwa nyumba leo, Kizito Joachim ametoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia kwa kazi kubwa aliyoifanya tangu kutokea kwa janga hilo mpaka sasa wanapokabidhiwa nyumba hizo.
"Tunakumbuka upendo wa Rais Dkt. Samia; hakika alikuwa mfariji mkuu na tunaendelea kumuombea kwa Mungu. Kwako pia Mheshimiwa Waziri Mkuu tunakushukuru wewe kwa kuzielekeza Wizara na wadau mbalimbali kuja kutunusuru kutokana na janga lile.”