Jaji Mkuu awataka Mahakimu wapya kuzingatia maadili na kubadili fikra

NA FAUSTINE KAPAMA
Mahakama Lushoto

JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Mahakimu 88 wapya kuzingatia maadili wanapotekeleza majukumu yao na kubadili fikra na mitazamo katika huduma za Mahakama.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza baada ya kuwaapisha Mahakimu 88 wapya kwenye hafla iliyofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto jana tarehe 30 Novemba, 2024.

Mhe. Prof. Juma alitoa wito huo jana tarehe 30 Novemba, 2024 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto baada ya kuwaapisha Mahakimu hayo na kisha kufungua mafunzo elekezi ambayo yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo hicho.

“Kubadili fikra na mitazamo sio kazi nyepesi na asilimia kubwa ya kazi ya Hakimu ni uadilifu. Unaweza kuwa na akili nyingi sana kupindukia, lakini ukazitumia zile akili kupindisha haki kwa sababu huna maadili,” alisema katika hafla hiyo iliyohuduriwa na Viongozi mbalimbali wa Mahakama.

Jaji Mkuu alibainisha kuwa kazi kubwa iliyofanywa na Mahakama ya Tanzania kama sehemu muhimu ya mageuzi na maboresho ya huduma za Mahakama ni kubadili fikra na kuondoa tamaduni na kawaida zilizozoeleka ambazo zilikuwa zikiathiri ufanisi, uwazi, weledi na uharaka wa utoaji huduma.

Alieleza kuwa fikra chanya inayosukuma maboresho na mabadiliko ni kutoa huduma bora zinazomlenga na kumjali mwananchi, kumfikishia huduma kwa wakati.

Mhe. Prof. Juma alibainisha pia kuwa kila baada ya takriban miaka mitatu, Mahakama imekuwa ikifanya tathmini ya maboresho, kutaka kujua ni kwa kiasi gani, maboresho yameleta huduma zinazowaridhisha watumiaji wa huduma za Mahakama.

“Kuweni tayari utendaji wenu kupimwa na mifumo ya teknolojia, kuweni tayari kupimwa kupitia maoni na mapendekezo ya wananchi kupitia programu za mrejesho na kituo cha huduma kwa mteja,” alisema.

Jaji Mkuu aliwahimiza Mahakimu hao kusoma kwa makini, ripoti ya utafiti iliyotayarishwa na Taasisi isiyo ya Kiserikali iitwayo Repoa, kuhusu kuridhika kwa watumiaji wa huduma za Mahakama 2023.

Alieleza kuwa ripoti ya 2023 ililenga kutoa mrejesho kwa Mahakama kuhusu huduma zake inazozitoa ikilinganishwa na matarajio ya watumiaji na watumishi tangu utafiti wa awali ulipofanyika mwaka 2015, 2019 hadi 2023.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya akitoa utambulisho wa Viongozi mbalimbali wa Mahakama waliohudhuria uapisho huo.


Sehemu ya Mahakimu wapya (picha mbili juu na picha mbili chini) ikifuatilia kwa karibu hotuba ya Jaji Mkuu baada ya kuapishwa.
Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja.
Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu wapya (juu na chini) baada ya kuapishwa.
"Ripoti ya Repoa iliwasilisha tathmini ya watumiaji kuhusu ubora wa huduma za Mahakama kwa kulinganisha ubora ulivyokuwa mwaka 2019 na 2023. Wajibu wenu Mahakimu wapya ni kuhakikisha viwango havishuki wakati Repoa watakapofanya utafiti ujao,” alisema.

Kwa mujibu wa utafiti huo, kuhusu hudma za Mahakama za Mwanzo kwa mwaka 2019, asilimia 57 ya wananchi walisema ni nzuri, asilimia 36 walisema wastani na asilimia sita walisema huduma ni mbaya, lakini mwaka 2023, asilimia 64 walisema huduma za Mahakama za Mwanzo ni nzuri, asilimia 31 walisema wastani na asilimia nne walisema huduma ni mbaya.

Kwa upande wa Mahakama za Wilaya, kwa mwaka 2019, wananchi asilimia 55 walisema huduma ni nzuri, wastani ilikuwa asilimia 37 na huduma mbaya ni asilimia saba, lakini mwaka 2023, utatifi unaonesha asilimia 62 ya wananchi walisema huduma zinazotolewa ni nzuri, wastani ilikuwa asilimia 33 na mbaya ilikuwa asilimia tatu.

Kuhusu Mahakama za Hakimu Mkazi, utafiti unaonesha asilimia ya wananchi waliosema huduma zinazotolewa ni nzuri ni asilimia 54, waliosema huduma ni za wastani ni asilimia 36 na waliosema huduma ni mbaya ni asilimia tisa kwa mwaka 2019, lakini kwa mwaka 2023, waliosema huduma nzuri walikuwa asilimia 62, wastani asilimia 33 na mbaya asilimia tatu.

Kwa upande wa Mahakama Kuu, utafiti unaonesha asilimia ya wananchi waliosema huduma ni nzuri ni asilimia 53 kwa mwaka 2019, waliosema huduma ni za wastani ni asilimia 40 na waliosema huduma ni mbaya ni asilimia tatu, lakini kwa mwaka 2023, waliosema huduma nzuri walikuwa asilimia 62, wastani asilimia 35 na mbaya asilimia mbili.

Aidha, kwa upande wa Mahakama ya Rufani, kwa mwaka 2019, asilimia ya wananchi waliosema huduma ni nzuri ni asilimia 82, waliosema huduma ni za wastani ni asilimia tisa na waliosema huduma ni mbaya ni asilimia tisa, lakini kwa mwaka 2023, waliosema huduma nzuri walikuwa asilimia 75, wastani asilimia 25 na mbaya asilimia nne.
Meza Kuu inayoongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu nyingine ya Mahakimu wapya (juu na chini) baada ya kuapishwa.
Viongozi wa Mahakama ya Tanzania waliohudhuria hafla hiyo wakiwa katika picha ya pamoja na Meza Kuu.

Viongozi wa Mahakama ya Tanzania waliohudhuria hafla ya uapisho na ufunguzi wa semina hiyo elekezi kwa Mahakimu 88 wapya ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Mary Levira na Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo.

Wengine ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Katarina Revocati Mteule, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya, Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. George Herbert, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Chiganga Tengwa na Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sundi Fimbo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news