Jeshi la Polisi latoa ufafanuzi madai ya mchezaji Bernard Morrison

DODOMA-Jeshi la Polisi limetoa ufafanuzi wa taarifa inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kumhusu mchezaji Bernard Morrison ikituhumu Kituo cha Polisi Mbweni ambapo limesema kuwa, taarifa hiyo kila mtandao unaongeza chumvi kutokana na kuwa na taarifa ya upande mmoja.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP David Misime amefafanua kwamba, Bernard Morrison, Machi, 2024 alifungua kesi ya wizi wa kuaminiwa katika Kituo cha Polisi Mbweni kuwa, akiwa Ghana alimtumia Abdul Rakeeb Mgaya kiasi cha shilingi milioni moja na laki tano (1,500,000) ili amkabidhi mdogo wake aliyemtaja kwa jina la Boat anayeishi hapa nchini akitafuta timu itakayo msajili lakini hakufanya hivyo.

DCP Misime amesema, baada ya malalamiko hayo aliyetuhumiwa alitafutwa na alipohojiwa alieleza ni kweli alitumiwa hizo fedha ili zisaidie kwenye gharama za kumsajili huyo mdogo wake, lakini ilishindikana kwa sababu hakuwa na kiwango cha kusajiliwa na timu aliyokuwa anahitaji.

Hata hivyo, alimtaka Bernard Morrison ampe muda atamrejeshea fedha zake. Pia alielezwa kulingana na ushahidi hakuna kesi ya jinai. Hivyo walielewana na kwa vile wote ni raia wa Ghana walikubaliana kulipana.

Juni 3,2024 iliripotiwa kesi ya kuharibu mali ambapo Bernard Morrison akiwa na mdogo wake na mtu mwingine walifika katika nyumba anayoishi Abdul Rakeeb na kuvunja geti kisha kuchukuwa kwa nguvu gari aina ya IST namba T239 DFM.

Bernard Morrison aliendelea kutafutwa bila mafanikio, lakini Abdul Rakeeb alifanikiwa kuliona gari hilo likiwa limeegeshwa sehemu na kulichukua na kulipeleka Kituo cha Polisi Mbweni.

Jeshi la Polisi limesema, Bernard Morriso anachotakiwa kufanya ni kuacha kujificha, kusema ukweli na kufika Kituo cha Polisi kuonana na uongozi ili sheria ichukue mkondo wake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news