DAR-Jukwaa la Wahariri Tanzania limeona na kupokea mabadiliko ya Baraza la Mawaziri Tanzania yaliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan leo Desemba 8,2024.
Katika mabadiliko hayo, Rais Samia pia ameihamisha Idara ya Habari kutoka Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na kuirejesha katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaana Michezo.
Sisi, Jukwaa la Wahariri Tanzania, tumepokea mabadiliko haya kwa moyo mmoja.
Awali tuliomba sekta ya habari ihamishwe katika wizara hii kutokana na kwamba ilionekana kumezwa na sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo, ambapo mawaziri wengi waliipa kisogo sekta ya Habari.
Mheshimiwa Rais imempendeza kuirejesha huko, tunaamini waliopewa dhamana hawataiweka kando sekta ya Habari kama ilivyokuwa awali.
Faraja tuliyoipata ni kwamba viongozi wakuu wote walioteuliwa kuongoza wizara hii mpya ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo-Waziri na Katibu Mkuu- wote ni waandishi wahabari kitaaluma. Tunaamini hawataipa kisogo sekta ya habari.
Tunawapongeza Waziri Prof.Palamagamba Kabudi aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Wizara hii mpya na Gerson Msigwa aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara hii mpya ya Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo,na kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali.
Tunampongeza na kumshukuru Thobias Makoba, aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, ambaye sasa ameteuliwa kuwa Balozi.
Tunamtakia kila la kheri katika utumishi wake mpya huko aendako. Sisi, Jukwaa la Wahariri Tanzania,tunaamini viongozi hawa walioteuliwa wataendeleza juhudi za kuwezesha uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kujieleza, na haki ya kupata habari.
Hii itakwenda sambamba na kufanyamapitio ya sera na kuboresha sheria za habari zinazoruhusu uhuru wa wanahabari na uhuru wakutoa maoni.
Tunawahakikishia wateule hawa ushirikiano wa hali ya juu katika utendaji wao wa kila siku natuko tayari muda wote kushirikiana nao kufanikisha Watanzania kupata haki ya kupata habaribila vizuizi. Hongera Prof. Kabudi, hongera Msigwa.