PWANI-Kamati ya Wataalamu ya Menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imefanya ziara ya kutembelea Mradi wa kufua Umeme wa Mwalimu Julius Nyerere (JNHPP) ulioko Rufiji mkoani Pwani.
Kamati hiyo imetembelea mradi wa kufua Umeme wa Julius Nyerere, tarehe 11 Desemba, 2024 kwa lengo la kujifunza na kupata uelewa wa pamoja wa namna mradi huo unavyoendeshwa.
Mara baada ya kuwasili katika eneo la mradi, Kamati ya Wataalamu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ilikutana na Wahandisi wanaosimamia mradi wa kufua Umeme wa Julius nyerere ambao waliwapitisha kwenye mada juu ya hatua za maendeleo ya mradi huo.
Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo, Mwandishi Mkuu wa Sheria, Bw. Onorius Njole ameushukuru Uongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuiruhusu Kamati ya Wataalamu ya Menejimeti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutembelea na kujionea mradi huo mkubwa wa kufua Umeme.
"Tunawashukuru Viongozi wa Ofisi yetu kwa kutupa fursa hii ya kutembelea mradi huu mkubwa wa umeme ambao tulikuwa tukiuona kwenye makaratasi,"amesema Mwandishi Mkuu wa Sheria.
Aidha, Mwandishi Mkuu wa Sheria ameipongeza Serikali kwa namna ilivyosimamia utekelezaji wa mradi kufua Umeme wa Julius Nyerere, ambao utasaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa Viwanda na matumizi ya Wananchi kwa ujumla.
"Mradi huu ni muhimu sana kwani utasaidia katika kuboresha na kukuza uchumi wa nchi," amesema Mwandishi Mkuu wa Sheria.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Uratibu na Ushauri wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bi. Neema Ringo amesema mradi huo mkubwa wa kufua umeme utaongeza upatikanaji na umeme hivyo kusaidia shughuli mbalimbali za maendeleo zinazotegemea umeme.
"Mradi ni mkubwa na unakwenda kubadilisha kabisa nchi yetu kwenye suala la uzalishaji wa umeme, tutakuwa na umeme wa kutosha ambao tunaamini utakuwa chachu ya maendeleo kwa Wananchi na Taifa kwa ujumla,"amesema Kaimu Mkurugenzi wa Uratibu na Ushauri.
Kwa upande wake mmoja ya Wahandisi wanaosimamia mradi wa kufua Umeme wa Julius Nyerere Eng. John Ndaki amesema mradi huo unatarajiwa kuwa na Mitambo tisa (9) ya kuzalisha umeme na hadi hivi sasa Mitambo mitano imanza kufanya kazi.
"Mradi huu utakuwa na mitambo tisa (9) ya kuzalisha umeme mpaka hivi sasa tuna mitambo mitano ambayo tayari inafua umeme, kwa ujumla wake mradi huu umefikia asilimia 99.35,"amesema Mhandisi Ndaki.
Kamati ya Wataalamu ya Menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiwa kwenye mradi kufua Umeme wa Julisu Nyerere, ilitembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Tuta kuu linalozuia maji (Main Dam), Mitambo ya Kuzalisha Umeme (Power House) na chumba maalumu cha kuendesha mitambo inayozalisha umeme (Control Room).