DAR-Askofu Mkuu Mwandamizi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jude Thaddeus Ruwa'ichi amesema, Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam litaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhamasisha watu walipe kodi kwa maendeleo ya nchi.
Akizungumza na Kamishna Mkuu wa TRA,CPA Yusuph Juma Mwenda alipomtembelea nyumbani kwake jijini Dar es Salaam ikiwa ni mwendelezo wa kuwashukuru walipakodi, Askofu Mkuu Ruwa'ichi amesema,suala la kulipa kodi na kukusanya kodi ni suala linalohusu maendeleo ya nchi na ni sehemu ya wajibu wa kiraia.
Askofu Mkuu Ruwa'ichi ameeleza kufurahishwa na mfumo wa ukusanyaji wa Kodi unaofanywa katika kipindi cha sasa na ukaribu uliopo baina ya Mamlaka hiyo na Wananchi.
"Kwa niaba ya Watanzania wenzangu niwapongeze kwa kazi kubwa mnayoifanya na kuwahakikishie kwamba kadiri ya nafasi na uwezo wetu tutajitahidi kuwahimiza watu wazingatie na waenzi wajibu wa kulipa Kodi kwa ajili ya maendeleo yao wenyewe.
"Nafurahi kwa msisitizo ulioweka kwamba katika kukusanya Kodi hambagui huyu wala yule, mnatafuta kuwatendea wote Haki, naomba hilo lidumishwe na litiliwe mkazo,"amesema Askofu Mkuu Ruwa'ichi.
Amesema TRA inafanya vizuri inapolenga kila raia alipe Kodi inayoendana na uwezo wake wa kulipa na kodi hiyo inatumika kwaajili ya watu wote kuleta Maendeleo bila kujali Itikadi zao na kuwa ataendelea kushirikiana na TRA.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa TRA Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema lengo la kumtembelea Baba Askofu Mkuu Ruwa'ichi ni kumshukuru kwa mchango wake katika kuhamasisha ulipaji wa Kodi huku wakitambua mchango wa Kodi unaotokana na Taasisi zilizopo chini ya Kanisa Katoliki.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema Disemba ni Mwezi wa kuwashukuru Walipakodi na kuzitaja baadhi ya Taasisi zilizopo chini ya Kanisa Katoliki ambazo zimekuwa na mchango katika Kodi kuwa ni Sekta za Elimu na Afya ambapo wakati mwingine wamekuwa wakisamehewa Kodi kulingana na sheria za Kodi.
"Wewe Baba Askofu umekuwa muhamasishaji mkubwa wa masuala ya Kodi na tumekuwa na ushirikiano na Taasisi za kanisa hivyo tumekuja kushukuru na kukuomba ushirikiano katika mwaka mpya ujao wa 2025 uendelee kutusaidia kuhamasisha" amesema Kamishna Mkuu Mwenda.
Kamishna Mkuu Mwenda amesema kulipa Kodi kwa maslahi ya Nchi ni jambo la kiimani maana Kodi hizo zinazokusanywa ndiyo zinaleta maendeleo ya Elimu, Afya na Miundombinu.
"Tunaheshimu Sana Taasisi za kidini maana nyuma yenu mna watu wengi hivyo tunaendelea kushirikiana nanyi kukusanya Kodi kwa Haki kuhakikisha kuwa hakuna anayeonewa na tunachokitaka ni kuhakikisha kunakuwa na usawa wa ushindani sokoni" Amesema Kamishna Mkuu Mwenda.
Amesema TRA ipo kuwasaidia Walipakodi ili walipe Kodi kwa hiari.