ARUSHA-Wananchi wilayani Karatu mkoani Arusha wamejitokeza kwa wingi kujipatia majiko ya gesi ya kilo sita (LPG) yanayotolewa na Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya Lake Gas kwa bei ya ruzuku ya 50%.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wameipongeza Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kuja na mkakati huo ambao wamesema utawasaidia kupunguza gharama walizokuwa wakitumia kununua mkaa.
Mkazi wa Kata ya Qurus, Neema Alfred amesema mkakati huo wa Serikali wa kusambaza majiko kwa bei ya ruzuku unakwenda kuwapunguzia adha ya kutembea mwendo mrefu kusaka kuni.
"Kijijini kwetu kuni hazipatikani ni hadi tutembee umbali mrefu; kwahiyo kupata haya majiko ya gesi na kwa bei nafuu ni neema kwetu," amesema Neema.
Elizabeth Fikalala kutoka Kiiiji cha Bashay alisema kijijini hapo upatikanaji wa kuni ama mkaa ni mgumu na kwamba wanalazimika kutumia gharama kubwa kunua mkaa hivyo ujio wa mradi huo ni mkombozi kwetu.
Naye Hassan Juma mkazi wa Kata ya Karatu ambaye anajishughulisha na uuzaji wa chipsi ameishukuru Serikali kwa kuwafikishia majiko ya gesi kwa bei ya ruzuku na kwamba jiko hilo linakwenda kumrahisishia kazi zake.
"Tunaishukuru Serikali kwa hili la mitungi ya gesi, mazingira yetu yanakwenda kuwa masafi na pia ni rahisi kutumia tofauti na kutumia mkaa," alisema Juma.
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 ambao ulizunduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mwezi Mei mwaka huu.