ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema,kushuka kwa thamani ya dola nchini ni faraja kubwa kwa uchumi, kwani kutapunguza ugumu wa gharama za maisha kwa wananchi.

Amesema, ni matarajio yake kushuka kwa dola kutasaidia pia kupungua gharama za baadhi ya mahitaji kwenye maisha ikiwemo bidhaa muhimu za chakula na mafuta.
Akizungumzia suala la uingizwaji wa bidhaa nyingi na athari za kupanda kwa dola, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kwamba, iliathiri sana uchumi wa nchi licha ya kuwa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa nchini zilifidia hasara hasa wakati wa mavuno akitolea mfano chakula ikiwemo mchele kwa kiasi ilipunguza kasi ya uagiziaji kutoka nje.
Wakati huo huo, Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Benki Kuu ya Tanzania kwa weledi wa kuendelea kuwahamasisha wananchi juu ya kubadilisha noti za zamani zinazoondoshwa kwenye mzunguko kwa matumizi yao ya kila siku.

Akizungumzia kuhusu kushuka kwa thamani ya dola nchini, Gavana Tutuba amesema ni hatua moja ya benki hiyo kuipandisha thamani na kuirejesha kwenye mzunguko wa soko, fedha ya ndani ambayo kwa kipindi kirefu ilishuka.
Pia,ametoa angalizo kwa wafanyabishara wote nchini pamoja na kuwajulisha Watanzania kwamba ni marufuku kwa mfanyabiashara yeyote kuuza ama kununua bidhaa kwa kutumia dola ama fedha yoyote ya kigeni.