ZANZIBAR-Mkuu wa Mkoa Kaskazini Unguja, Mhe. Mattar Zahor Masoud, amesema Serikali kwa nia njema imeruhusu kuwepo asasi za kiraia ili kusaidia juhudi za Serikali katika kuleta maendeleo na sio vinginevyo.
Akizungumza na Masheha wa mkoa huo ofisini kwake Mkokotoni, amesema zipo asasi nyingi za kiraia zimekuwa zikifanya vizuri katika kuongeza nguvu za kuiwezesha jamii kuweza kujiendesha na kujikimu kimaisha.
Hivyo amewataka masheha hao kutosita kutoa taarifa endapo watabaini baadhi ya asasi hizo zinakwenda kinyume na malengo ya kuanzishwa kwake.
Kwa upande wake Mrajis wa Jumuiya zisizo za kiserikali Ahmed Khalid Abdullah, amesema asasi za kiraia endapo zitatekeleza vyema majukumu yake manufaa makubwa yatapatikana hasa katika masuala ya uzalishajimali.
Akiwasilisha mada ya majukumu ya masheha katika usalama wa shehia, Mkufunzi Bi Zuhura Salum Rashid, amesema masheha wanalazimika kufatilia kwa karibu mambo yanayojitokeza katika shehia zao.