DAR-Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, Tundu Lissu ametangaza nia ya kuwania Uenyekiti wa chama hicho Taifa huku akitumia uzoefu wa wakongwe katika siasa kumkosoa Freeman Mbowe kwa kung'ang'ania madaraka.
Ameyasema hayo leo Desemba 12,2024 katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kupitia mkutano uliojumuisha wawakilishi kutoka maeneo mbalimbali nchini.
"Tangu, na mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kutoka kwa baadhi ya wanachama na viongozi wa chama chetu ya kunishawishi kutaka kugombea nafasi ya Uenyekiti wa chama chetu.
"Mara zote nimechukulia ushawishi huo kuwa ulikuwa na nia njema ya kuhakikisha kwamba, tunaendeleza na kuimarisha utamaduni wa kubadilishana uongozi na madaraka ya uongozi ndani ya chama chetu uliowekwa na viongozi wakuu waanzilishi wa chama chetu yaani Mzee Edwin Mtei na marehemu Mzee Bob Makani.
"Wazee wetu hawa walikuwa wasomi waliosomeshwa katika mila na desturi za kisasa za Kiingereza.
"Bila shaka walikuwa wanafahamu na walizingatia funzo la kutong'ang'ania madaraka lililotolewa na Oliver Cromework kwa wabunge wa Uingereza mwaka 1953 wakati wa vita kati ya wafuasi wa Bunge na wafuasi wa Mfalme Charles I.
"Hilo funzo la kutong'ang'ania madaraka kwa maneno ya Oliver Cromework yalikuwa hivi, Oliver Cromework alikuwa mwanamapinduzi wa mwaka huo nchini Uingereza.
"Aliwaambia hivi, wabunge waliokuwa wameng'ang'ania madaraka, waliokuwa wamekaa bungeni bila uchaguzi.
"Alisema maneno yafuatayo,mmekaa hapa kwa muda mrefu sana kwa mazuri yoyote ambayo mmekuwa mkifanya, ondokeni. Ninasema, ili tumalizane nanyi kwa jina la Mungu nendeni zenu.
"Kwa sababu ya ufahamu wao wa historia hii Mzee Mtei na Mzee Makani hawakutaka kukaa madarakani mpaka watakapolazimishwa kuondoka kwa aibu.
"Waliandaa utaratibu wa kuondoka madarakani kwa hiari yao na kwa kutumia taratibu za kikatiba.
"Kwa msiokuwa na kumbukumbu za urithi wa wazee wetu hawa,Mzee Mtei alitumikia nafasi ya Mwenyekiti Taifa kwa kipindi kimoja cha miaka mitano.
"Na alistaafu uongozi mwaka 1998 akiwa na umri wa miaka 66 kama ambavyo ameeleza katika kitabu cha historia ya maisha yake kutoka mchunga mbuzi hadi Gavana.
"Mara baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 akiwa na umri wa miaka 63, Mzee Mtei alitambua haja ya alichokiita damu changa na mpya, yaani waliokuwa wabunge wa Chadema ambao hawakuwa wajumbe wa kamati kuu kuchukua dhamana ya uongozi wa chama.
"Hivyo, alianzisha mchakato wa mabadiliko ya katiba ya chama ili kuwezesha damu changa hiyo kuwa wajumbe wa kamati kuu wa moja kwa moja.
"Na hivyo, ndivyo ilivyotokea kwamba Mzee Bob Makani aliyekuwa Katibu Mkuu mwanzilishi wa Chadema alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama huku Makamu Mwenyekiti akiwa Dkt.Willbroad Slaa.
"Kwa upande wake Mzee Bob Makani alishikilia kipindi cha madaraka kwa muhula mmoja hadi mwaka 2003 na nafasi yake kuchukuliwa na Freeman Mbowe.
"Nafasi ya Katibu Mkuu ilichukuliwa na Dkt.Slaa huku Dkt.Kaburu akipandishwa cheo na kuwa Makamu Mwenyekiti.
"Ni muhimu kusisitiza kwamba, mabadiliko yote hayo ya uongozi wa juu wa chama yalifanyika kwa njia ya uchaguzi kwa mujibu wa katiba ya chama.
"Haijatotekea katika historia yote ya chama chetu kwamba uongozi wa juu unatolewa kama zawadi ama fadhila kutoka kwa kiongozi au viongozi waliopo madarakani.
"Huu ndiyo urithi wa viongozi na waanzilishi wa chama chetu tunaopaswa kuuenzi na kuuendeleza."
Tags
Habari