KIGOMA-Ujenzi wa maabara tatu za Sayansi katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kakonko mkoani Kigoma umeleta hamasa kubwa ya kitaaluma kutokana na kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia.

Mkuu wa shule hiyo, Anatoria Paul Nkabo, alisema kukamilika kwa mradi huu kutaongeza hamasa ya wanafunzi kufanya vizuri zaidi katika masomo ya sayansi kutokana na mazingira bora na rafiki ya kujifunzia kwa vitendo.

Mwalimu wa Kemia na Biolojia, Nikolous Kayombo, aliongeza kuwa awali walifundisha masomo hayo kwa nadharia pekee, lakini sasa, kupitia maabara hizi, wanafunzi wataweza kujifunza kwa vitendo, hivyo kuongeza uelewa na ufaulu wao.
Wanafunzi Zulfa Twaha (Kidato cha Kwanza), Happines Amosi (Kidato cha Tatu), na Sharifat Hamad walitoa shukrani zao kwa UNICEF na TEA kwa kuwapatia maabara hizi muhimu. Walibainisha kuwa maabara hizi zinawawezesha kufanya majaribio mengi ya masomo ya sayansi, jambo linalochochea mafanikio yao kitaaluma.
Mbali na maabara, TEA pia ilitoa ufadhili wa ujenzi wa bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 120 mwaka 2022/2023, kwa gharama ya zaidi ya TZS milioni 142.9.

Shule ya Wasichana Kakonko iliyoanzishwa mwaka 2022 ina jumla ya wanafunzi 274, na mwaka 2025 inatarajia kudahili wanafunzi wengine 100 wa kidato cha kwanza, jambo linaloashiria maendeleo endelevu shuleni hapo.