MTWARA-Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika vya Kifedha kutoka Tume ya Taifa ya Maendeleo ya Vyama vya Ushirika (TCDC), Bw. Josephat Kisamalala, amewataka viongozi wa Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) kuhamasisha wanachama wengi wajiunge na vyama hivyo ili kuendana na shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika Kanda ya Kusini.
Amesema hayo wakati akizungumza mwishoni mwa mafunzo ya siku mbili kwa viongozi na wafanyakazi wa SACCOS katika mikoa ya Mtwara na Lindi walioshiriki katika mafunzo kuhusu Mfumo wa Taarifa za Mikopo yaliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania.
“Kunahitajika hamasa ya kutosha ili watu wapende kuanzisha na kujiunga na SACCOS. Kuna shughuli nyingi sana za kiuchumi katika mikoa ya kusini ambazo zinahitaji ujumuishi katika huduma za fedha kupitia taasisi kama hizi,” amesema Bw. Kisamalala.
Aidha, kiongozi huyo amezitaka SACCOS nchini kujiunga na mfumo wa taarifa za mikopo kwa ajili ya kupata taarifa za mikopo ya wateja wao ili waweze kuwahudumia wananchi sawasawa na taarifa hizo zinavyoeleza na hatimaye kupunguza mikopo chechefu.
“Tunafanya biashara ya fedha, wanachama wetu pia wanakopa kwingine; ili taasisi zetu ziendelee kuwa endelevu, ni vizuri kujua taarifa za wakopaji. Ni muhimu kutumia mifumo hii ya taarifa za wakopaji kujiridhisha kuhusu tabia za wakopaji ili kukwepa kupata hasara,” amesema.
Amesema kupitia taarifa za mikopo zinazopatikana katika kampuni zinazochakata taarifa za wakopeshaji za Credit Info Tanzania na Dun & Bradstreet Tanzania, SACCOS zinaweza kuwa na uhakika za watu wanaotaka mikopo kwao.
“Watu ambao hawakopesheki wanaweza kugundulika mapema. Mfumo wa taarifa za mikopo unakupa picha. Kwa mfano, kama mteja ameshindikana kwenye taasisi kubwa kama tatu, sisi tulio kwenye ngazi ya wilaya tunaweza kumpata?,” aliuliza Bw. Kasamalala akielezea umuhimu wa kutumia taarifa za wakopaji.
Akifunga mafunzo hayo ambayo yalianza tarehe 2 Desemba kwa kampuni zinazotoa huduma ndogo za fedha, benki na taasisi za fedha na mwishoni SACCOS, Meneja Usimamizi Taasisi Maalum za Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Bi. Suzan Katabi, amesisitiza SACCOS zinaweza kujua tabia za wateja wao kupitia mfumo wa taarifa za mikopo.
“Ni vyema tukajitahidi kutumia mifumo iliyopo ya taarifa za mikopo ili fedha za watu ziendelee kuwa salama,” amesema Bi. Katabi.
Aidha, amewataka washiriki wa mafunzo haya kutumia elimu waliyoipata kuwafikia wengine ili SACCOS katika mikoa ya Mtwara na Lindi ambayo uchumi wake unakua kwa haraka ziweze kuongezeka.
Katika mafunzo haya, washiriki walipata mada kutoka Benki Kuu ya Tanzania kuhusu sheria na kanuni zinazohusu matumizi ya taarifa za mikopo zinazopatikana katika kanzidata za kampuni za kuchakata taarifa za mikopo na kampuni za kuchakata taarifa hizo za Credit Info na Dun & Bradstreet Tanzania, ambazo zilieleza namna kampuni hizo zinavyofanya kazi na jinsi wadau mbalimbali wanavyoweza kushirikiana nazo kwa kupeleka taarifa na kutumia taarifa za wakopaji wanazozichakata.