DAR-Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema zaidi ya trilioni nane zimetolewa kwa wanufaika 830,000 nchi nzima tangu ilipoanzishwa, huku ikijiandaa kuadhimisha miaka 20 mwakani.
Pia, imesema kwa mwaka huu wa fedha, wamepanga mikopo kwa wanufaika 245,799 nchi nzima ambao wamepangiwa kutumia Sh bilioni 787. Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Dkt.Bill Kiwia amesema hayo Dar es Salaam wakati akizungumzia maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa bodi hiyo.
Akizungumza na wanahabari, Dkt.Kiwia alisema katika kuadhimisha miaka yao 20, wameandaa mbio za marathoni, kongamano na kliniki ya utoaji huduma kwa wanafunzi na wazazi katika mikoa saba Tanzania Bara na Zanzibar.
“Maadhimisho haya yatakuwa na matukio ya muhimu, kwanza kutakuwa na mbio za hisani, hii inaitwa HESLB Marathon, pili kutakuwa na maonesho na huduma mikoani yaani tutakuwa na kliniki tutazungumza na wadau wetu ambao ni wanafunzi watarajiwa hata wazazi,” alisema Dkt.Kiwia.
Tags
Kurasa za Magazeti
Kurasa za Mbele na Nyuma za Magazeti
Magazeti
Magazeti ya Leo
Magazetini
Magazetini leo
Yaliyojiri Magazetini Leo