Mahakama isiwe upanga wa dhuluma

ZANZIBAR-Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman amesema,hadhi na heshima ya Mahakama hailetwi na uzuri wa majengo pekee, bali pia misingi imara ya haki na uadilifu.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo akiwa mgeni rasmi katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mkoa wa Kaskazini Pemba huko Kinyasini Wilaya ya Wete.

Ameeleza kuwa, Mahakama isiyozingatia haki na uadilifu, hata iwepo na jengo zuri kiasi gani, inageuka kuwa ni ‘upanga muovu uliokosa hekima’, na hivyo bila ya kurefusha maneno, utaitwa ‘upanga wa dhuluma’.

Amesema, Serikali ya Zanzibar imekuwa na mkakati maalum wa ujenzi wa majengo ya kisasa ya Ofisi za Mhakama ili kuimarisha mazingira bora ya kufanyia kazi, kwa lengo la kuchochea utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Zanzibar; Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla, amepongeza Serikali ya Awamu ya Nane, kwa kuipa kipaumbele Sekta yote ya Muhimili huo wa Dola, ikiwemo uimarishaji wa miundombinu yake.
Ametaja juhudi hizo kuwa ni pamoja na ujenzi wa majengo saba ya Mahakama kisiwani Pemba ili kuimarisha utoaji wa huduma mbalimbali za kisheria.

Sambamba na kufanikisha Andiko na Ombi la Mradi kwa Benki ya Dunia ili kupatiwa Mkopo kwa ajili ya kuimarisha Utendaji wa Muhimili huo muhimu kwa Kipindi cha Miaka Mitano.

Akitoa salamu za Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Kaimu Waziri wa Wizara hiyo, ambaye ni Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili, na Mifugo, Mhe. Shamata Shaame Khamis, amesema, Serikali itahakikisha inasimamia Bajeti na Maelekezo, ili kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Viongozi mbalimbali wa Serikali, Vyama vya Siasa, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Jaji Dhamana wa Mahakama Kuu Zanzibar, Wabunge wa Bunge la Jamhuri, Dini, Jamii, Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia, Watendaji wa Taasisi za Kisheria, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama wamehudhuria hapo wakiongozwa na Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Hassan Othman Ngwali; na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Bi Salama Mbarouk Khatib.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news