Mahakama ya Tanzania ipo tayari kukosolewa,siyo kubezwa-Jaji Mkuu

NA FAUSTINE KAPAMA
Mahakama Lushoto

JAJI Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewasihi Wadau wa Mahakama kuwa makini na kauli wanazozitoa zinazolenga kubeza mfumo mzima wa utoaji haki nchini.
Mhe. Prof. Juma ametoa wito huo leo tarehe 30 Novemba, 2024 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kwenye hafla ya uapisho na ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa Mahakimu 88 wapya.

“Wito wangu kwa wadau wetu ni kwamba watofautishe kukosoa na kubeza. Mahakama tuko tayari kukosolewa ila hatuko tayari kubezwa kwa lengo tu la kuchafua taswira ya Taasisi yetu na kuwakatisha tamaa Majaji na Mahakimu ambao wanafanya kazi muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa letu,” amesema.

Jaji Mkuu amerejea ‘video clip’ iliyosambazwa mitandaoni hivi karibuni ikimnukuu Mwananchi mmoja akieleza kuwa hukumu zinazotolewa siku hizi na kuchapishwa kwenye mtandao wa Mahakama, TanzLII, hazina kitu chochote, huku akidai pia kuwa Mahakama ya Rufani ina Majaji ‘Spoilers” na Majaji wa Serikali.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) akizungumza kwenye hafla ya uapisho na ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa Mahakimu 88 wapya leo tarehe 30 Novemba, 2024 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.

Sehemu ya Mahakimu wapya ikila kiapo (juu na chini.

Hata hivyo, Jaji Mkuu anasema wapo Wananchi wengine ambao wana maoni tofauti na wamejitokeza kuweka wazi kuwa, wameona maamuzi ya Mahakama ya Tanzania yamewasaidia kwa vitendo katika kuboresha huduma za utoaji haki na kufanya tafiti mbalimbali.

“Kwa mfano, msongamano katika magereza unagusa haki kadhaa za binadamu. Majaji na Mahakimu huona kazi zao zinathaminiwa na zina faida kubwa zaidi ya maamuzi yaliyokusanywa na Mwananchi huyu mwaka 1997 (miaka 27 iliyopita),” amesema.

Mhe. Prof. Juma ameeleza kuwa wiki chache zilizopita alitembelewa ofisini kwake na Kamishna Jenerali wa Magereza, Jeremiah Yoram Katungu na yeye kwa uzoefu wake wa hali ya sasa akilinganisha na zamani alisema uwezo wao wa kuhifadhi Wafungwa na Mahabusu ni 29,90,2 lakini kutokana na ufanisi wa Mahakama kuendesha mashauri kwa teknolojia kwa sasa wana Mahabusu 27,000 tu na akaipongeza Mahakama kwa maboresho hayo.

Jaji Mkuu amebainisha pia kuwa amebaini kuwa hata yule Mwananchi aliyekuwa analalamikia ubora wa hukumu za Mahakama bado ametupa fursa nzuri ya kujua nini cha kuelimisha jamii. Kwa hiyo, amesema Mahakama lazima iongeze mawasiliano na Umma ili kujitangaza na kueleweke na wananchi, kwa wale ambao wako tayari kuelewa.

Mhe. Prof. Juma amesema kazi ya Jaji au Hakimu ni kutoa maamuzi au hukumu ambayo hutatua mgogoro baina ya walioleta mgogoro wao mahakamani, hivyo suala la kupenda au kutopenda uamuzi ni utashi wa anayeguswa na hukumu au msomaji.

“Kwa mantiki hii, hata mtu mmoja kuona kuwa hukumu ni bora au sio bora inategemea anaangalia kwa jicho lipi, kwa lengo lipi na kwa hisia gani na hii husababisha kuwa na mwelekeo wa kutathmini kwa namna tu ya kudhania (subjectively) kwa jinsi yeye anavyodhania,” amesema.
Sehemu ya nyingine ya Mahakimu wapya (juu na chini) ikila kiapo mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto).
Sehemu ya nyingine ya tatu ya Mahakimu wapya (juu na chini) ikila kiapo mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto).
Hivyo ametoa wito kwa Watanzania kuwa waungwana kukiri kwamba, zama za kukusanya maamuzi na kuchapisha vitabu vyenye maamuzi ya Majaji zimepitwa na Mapinduzi ya Teknolojia na kwamba kupandishwa maamuzi yote na kupatikana kwa urahisi kupitia mtandao wa TANZLII ni matunda ya maboresho yanayoendelea.

“Huu mfumo wetu wa TANZLII unasifiwa duniani na unatembelewa kuliko mifumo mingine yote duniani. Mahakama ya Tanzania, kwa kushirikiana na AfricanLII na Laws Africa, wameanzisha Sheria Mkononi kusaidia kupatikana kwa hukumu hata bila kuwa na mtandao. Watanzania tujivunie cha kwetu na kama kuna hoja za kuboresha, basi tufanye hivyo kwa kutumia njia sahihi baada ya kuwa na ushahidi wa kisayansi usiotiliwa shaka,” amesema.

Akizungumzia suala la Majaji Spoilers au Majaji wa Serikali, Jaji Mkuu amekiri hii ni mara ya kwanza kwake kusikia kutoka kwa yule Mwananchi mtaalamu wa sheria kwamba Mahakama ya Rufani, katika upangaji wa Majopo, na katika kufikia maamuzi, kulikuwa na Jaji mmoja mahsusi wa Serikali mwenye kazi moja tu, ya kuharibu (spoiler).

“Kwa bahati nzuri bado wapo Majaji wa Rufani wastaafu, kwa mfano Jaji Januari Msoffe na Jaji Edward Rutakangwa, ambao walihudumu kama Wasajili zamani hizo, ambao wanaweza kutoa mwanga zaidi…
Sehemu ya nyingine ya nne ya Mahakimu wapya (juu na chini) ikila kiapo mbele ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto).



Sehemu ya Mahakimu wapya ikitia sahihi kwenye kiapo hicho.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitia sahihi kwenye moja ya viapo hivyo.
Viongozi wa Mahakama ya Tanzania waliohudhuria hafla ya uapisho na ufunguzi wa semina hiyo elekezi kwa Mahakimu 88 wapya. Kutoka kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Mary Levira, Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dkt. Mustapher Mohamed Siyani, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Katarina Revocati Mteule na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel.

“Nimgependa pia kumjulisha yule Mwananchi aliyekuwa analalamika kuwa ubora wa hukumu za Mahakama unaharibiwa na “spoilers” kuwa hakujawahi kuwa na hao “spoilers,” na Mahakama ya Tanzania ina Majaji wa Mahakama Kuu na Majaji wa Mahakama ya Rufani. Hakuna Majaji wa Serikali,” Jaji Mkuu amesema.

Hivyo, amewaomba Majaji na Mahakimu kutokatishwa tamaa na kauli hasi, au kejeli watakazokutana nazo, bali watumikie Watanzania kwa misingi ya uwazi, uweledi na maadili mema bila upendeleo katika utoaji haki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news