ARUSHA-Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeanza usambazaji wa majiko ya gesi (LPG) ya kilo sita kwa bei ya ruzuku Wilayani Longido Mkoani Arusha ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034.
Hayo yameelezwa Desemba 3, 2024 wilayani Longido na Mhandisi wa Miradi wa REA, Kelvin Tarimo wakati wa mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Longido na Naibu Waziri wa Madini, Mhe. Dkt. Steven Kiruswa wa kuelezea utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya Serikali wilayani humo.
"Tupo hapa Wilayani Longido kwa ajili ya kutoa elimu na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwa ni pamoja na kuanza rasmi uratibu wa mradi wa kusambaza na kuuza majiko ya gesi (LPG) ya kilo 6 ambapo kwa Wilaya ya Longido pekee jumla ya majiko 3,255 yatauzwa kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50," amesema Mhandisi Tarimo.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi, Mhe. Kiruswa ameipongeza REA kwa kutekeleza miradi yake kwa ufanisi ambapo alisema kwa wilaya hiyo ya Longido hadi sasa vijiji vyote 51 vimefikishiwa umeme na kazi inaendelea ya kuunganisha vitongoji.
Mhandisi Tarimo amesema Wakala wa Nishati Vijijini unalo jukumu la kuhakikisha Watanzania wanaachana na matumizi ya nishati isiyo safi na salama kama ambavyo imeelekezwa katika Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Aidha, ametoa rai kwa wananchi kutumia umeme kujiletea maendeleo hasa ikizingatiwa kuwa umeme ni fursa.
"Wakala unatoa rai kwa wananchi kutumia umeme kujiletea maendeleo ya kiuchumi na pia kupikia kwani umeme ni moja kati ya nishati rafiki kwa matumizi ya kupikia," amesisitiza.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi wa Longido wamepongeza jitihada za Serikali za kuwasambazia nishati safi ya kupikia mbayo wamesema ni hatua nzuri ya kulinda afya zao na mazingira kwa ujumla.
Sinyati Yohana mkazi wa Kata ya Ketumbeine amemshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaondolea kero wananchi wa Longido hususan wanawake na watoto ya kutembea umbali mrefu kusaka kuni kwa ajili ya kupikia.
Naye Larasha Lulungen mkazi wa Kata ya Matale amesema uwepo wa nishati safi ya kupikia wilayani hapo ni hatua ya kupongezwa kwani inakwenda kuimarisha afya za wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia kuni kupikia.
"Tulikuwa tunasikia tuu nishati safi lakini leo tumeelimishwa na pia tumeshuhudia majiko ya gesi yaliyotolewa na Serikali kwa ruzuku," amesema Lulungen.
Wakala wa Nishati Vijijini unaendelea kutekeleza mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa lengo la kuhakikisha ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya wananchi wawe wameachana na matumizi ya nishati zisizo safi na salama.