IRINGA-Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema ili kuinua viwango vya tafiti za vyuo nchini, vyuo vya elimu ya juu havina budi kuendelea kuwekeza katika tafiti hususan za sayansi na teknolojia na kuhimiza ubunifu katika ufundishaji na ujifunzaji.
Makamu wa Rais amesema hayo aliposhiriki Mahafali ya 27 ya Chuo Kikuu cha Iringa (UoI) yaliyofanyika katika viwanja vya chuo hicho mkoani Iringa.
Ametoa wito kwa sekta binafsi kuunga mkono jitihada hizo kwa kuendelea kushirikiana na vyuo vya elimu ya juu kwa kufadhili tafiti, kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa fani mbalimbali, kuanzisha vyuo vya elimu ya juu, kushirikiana na vyuo vya elimu ya juu kwa kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo na mafunzo kazini.
Aidha Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) katika ufundishaji na ujifunzaji katika ngazi ya elimu ya juu. Amesema uwekezaji katika mifumo ya TEHAMA utawezesha ufundishaji wa baadhi ya masomo kwa njia ya mtandao na hivyo kuongeza idadi ya watanzania watakaopata elimu ya juu.
Ameongeza kwamba ufundishaji kwa njia ya mtandao utapunguza changamoto ya uhaba wa walimu ambapo mwalimu mmoja anaweza kuwafikia wanafunzi wengi kwa wakati mmoja.
Halikadhalika, Makamu wa Rais ametoa wito kwa Vyuo Vikuu na taasisi nyingine za elimu ya juu nchini kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, ili kufundisha masomo na ujuzi muhimu unaokosekana nchini pamoja na ujuzi wenye wataalamu wachache kama vile madaktari bobezi wa upasuaji wa neva (neurosurgeon), upandikizaji wa uroto (none-marrow transplant), upandikizaji wa figo (kidney transplant), uhandisi wa roboti (robotic engineering), fizikia ya Nyuklia (nuclear physics), matumizi ya akili mnemba (application of artificial intelligence) na nano teknolojia (nano technology).
Vilevile amewasihi wahitimu kutumia fursa mbalimbali zilizopo nchini kama vile sekta za kilimo biashara, ufugaji wa samaki kwa kutumia vizimba, nishati jadidifu, matumizi ya teknolojia za kidijitali na TEHAMA, unenepeshaji wa mifugo, ufugaji wa nyuki, biashara na viwanda vidogo vidogo ili kujipatia mitaji.
Aidha, amewatahadharisha wahitimu kuhusu tabia ya kupenda mafanikio ya haraka pasipo kufanya kazi kwa bidii.
Makamu wa Rais amepongeza jitihada za Kituo cha Ujasiriamali na Ubunifu na atamizi ya Kiota (Kiota Innovation Hub) ya Chuo Kikuu cha Iringa kwa kutoa mafunzo ya ubunifu na ujasiriamali kwa wanafunzi na wajasiriamali.