Mameneja rasilimali watu Zanzibar wafundwa

ZANZIBAR-Kamishna wa Kazi na Uchumi katika Kamisheni ya Kazi Zanzibar, Rashid Khamis Othman amewataka mameneja rasilimali watu kuja na mbinu za kupunguza migogoro ndani ya kazi.
Akifungua semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo wadau hao iliyoandaliwa na umoja wa mameneja wa rasilimali watu Zanzibar, huko hoteli ya Madinatul Al Bahr alisema, uzoefu unaonesha kuwa migogoro ya kazi haitamalizika kutokana na kuwepo kwa migongano ya maslahi kati ya mwajiri na mwajiriwa, lakini ni vyema kutafuta namna ya kupunguza uwepo wa matukio hayo.

"Suala la migogoro kazini haliepukiki na maofisa hawa wana kazi ngumu ya kumridhisha mwajiri bila kuathiri kaki za mwajiriwa, ni vyema kuja na mbinu za kuweka usawa katika hali hiyo ili tusichangie kutokea kwa migogoro maeneo ya kazi."

Aidha, aliwashauri kuwa na majadiliano ya pamoja kati ya mwajiri na mwajiriwa ili kuwasaidia kupunguza migogoro katika maeneo yao ya kazi.

"Asilimia 90 ya migogoro inayotokea maeneo ya kazi inatokana na kuwa kila mmoja kati ya mwajiri na mwajiriwa anatamani kupata yeye zaidi na kuona anaonewa pale mrasilimali watu anapofanya wajibu wake kwa mujibu wa sheria."

Mbali na hayo aliwashauri kuendeleza semina kama hizo ili kuwajengea uwezo wa kutatuwa migogoro pale inapotokea bila kufika kitengo cha usuluhishi na migogoro, kutathmini na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zao na kubadilishana uzoefu wa kiutendaji.
Alitumia fursa hiyo kuwaonya waajiri wanaokwenda kinyume na sheria za kazi na kusema kuwa, siku za karibuni watafanya ukaguzi na kuchukua hatua za faini ya papo kwa papo kwa watakaobainika kuwa na makosa hayo kwa lengo la kuwalinda waajiriwa.

Aliyataja baadhi ya makosa hayo kuwa ni pamoja na kuruhusu mgeni kufanya kazi bila kibali, kuwa na mfanyakazi asie na mkataba, na kulipa chini ya kiwango cha mshahara kilichoelekezwa.

Mwenyekiti wa Umoja wa Mameneja Rasilimali watu Zanzibar, Omar Hassan Kigwama alisema, lengo la kikao hicho ni kujadiliana namna ya kunyanyua ujuzi wa watendaji hao katika kukabiliana na migogoro maeneo ya kazi.

Alisema,  inafahamika kuwa wataalamu hao wanakabiliwa na changamoto hasa ukizingatia wanafanyakazi ya utatu na kuwaomba kuzitumia changamoto hizo kama fursa ya kupiga hatua katika utendaji wao.

“Mameneja wanafanyakazi ya kuwaangalia wafanyakazi na wakati huo huo kulinda maslahi ya waajiri, endapo meneja atajitolea kusimamia maslahi ya mwajiri ama mfanyakazi pekee lazima migogoro itatokezea."

Kwa upande wake Katibu wa umoja huo, Abass Khamis Mussa alisema,  semina hiyo inalenga kuwakumbusha mameneja rasilimali watu juu ya kujua mipaka ya mwajiri na mwajiriwa ili kupunguza migogoro maeneo ya kazi.

Aidha,alieleza kuwa semina hiyo itawasaidia wataalamu hao kujua mbinu za kutatua migogoro maeneo yao ya kazi bila kwenda vitengo vya utatuzi wa migogoro.

Akiwasilisha mada katika semina hiyo mchambuzi na mhadhiri kutoka chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar SUZA, Prof. Khalfan Salim Suleiman, alieleza kuwa migogoro ya kazi inaendelea kutokea kwasababu baadhi ya mameneja rasilimali watu hawana utaalamu wa kazi hiyo hali inayopelekea kutotekeleza vyema majukumu yao.

“Kuna umuhimu wa mamaneje kujua majukumu yao haki na wajibu wa mwajiri na mwajiriwa ili kuwasaidia kufanyakazi bila upendeleo na kuepusha migogoro ndani ya kazi.”

Aliwataka wataalamu hao kujipambanua kwa kuongeza utaalamu na kuwa katikati baina ya mwajiri na mwajiriwa bila kuwa na upendeleo wakati wa kusimamia majukumu yao.

Prof.Suleiman aliwashauri mameneja rasilimawatu kuwa na mpango wa kuwahamasisha na kuwapa motisha wafanyakazi wanaotekeleza vyema majukumu yao ili kuongeza hamasa ya utendaji na kupunguza migogoro.

Nao washiriki wa mafunzo hayo akiwemo Vanesa Samoo alisema semina hiyo imewajengea uwezo na kupata mbinu mpya za kupunguza migogoro na ikitokea kuimaliza katika taasisi zao bila kushirikisha maofisa kazi.

Aidha,kwa niaba ya wataalamu wenziwe aliahidi kubadiilika kutokana na waliyojifunza katika semina hiyo.

Katika semina hiyo iliyowashirikisha mamaeneja rasilimali watu wa taasisi mbalimbali na maofisa kazi mada mbalimbali ziliwasilshwa na kujadiliwa ikiwemo namna ya kutatua migogoro bila kufika wizara ya kazi, na namna ya kumshawishi mwajiri kutoa hakiza wafanyakazi wake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news