Mawakili watajwa kikwazo kesi ya wanandoa Bharat Nathwan na Sangita Bharat

DAR-Mawakili wa utetezi katika kesi ya tuhuma za kujeruhi na kutoa lugha za matusi inayowakabili wanandoa Bharat Nathwan (57) na Sangita Bharat (54) wamendelea kuchelewesha kesi hiyo kwa kutokufika mahakamani bila kuwasilisha vielelezo kuhusu sababu za wao kutofika mahakamani.
Hali hiyo ilimkasirisha wakili wa serikali na hakimu kutokana na kujirudia rudia kwa tukio hilo na pia kuchelewesha kumalizika kwa kesi hiyo kwa wakati.

Hakimu Mkazi Mkuu Aaron Lyamuya wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam amemtaka Wakili Edward Chuwa na Gabriel Mnyele kuwasilisha nyaraka mahakamani kuonesha kama kweli walikuwepo Mahakama Kuu.

Hakimu Lyamuya alifikia hatua hiyo jana baada ya mshtakiwa Nathwan kuieleza mahakama kwamba amepata taarifa kutoka kwa wakili wake Chuwa kwamba yupo Mahakama Kuu mbele ya Jaji Hemed na pia Mnyele yupo safari mkoani Dodoma kwenye kikao cha mahakama (session).

Baada ya Nathwan kudai hayo, Wakili wa Serikali Faraji Ngukah alidai kuwa hawana pingamizi na taarifa hiyo ya mawakili, lakini ni tararibu za mahakama kwamba kama mtu anapata udhulu kwa busara anatakiwa awasilishe mahakamani nakala ya wito.

“Kama huyu tunaelezwa yupo Dodoma basi nyaraka ilitakiwa ioneshe hivyo, ili Mahakama iweze kujiridhisha kwamba mawakili hawa wapo Mahakama Kuu, kwa hiyo siku ya kesi wanatakiwa kuleta ushahidi.

“Sio kama hatuwaamini, lakini tangu mwanzo hawa wenzetu wamekuwa na shida hii ni kama wanapoteza muda wa mahakama tunaomba Mahakama itoe maelekezo juu ya hili,”alidai Ngukah.

Pia, aliweka wazi kwamba hata yeye ametoka Mahakama Kuu kwenye kesi ya tuhuma za ugaidi namba 61 ya mwaka 2022 Jamhuri dhidi ya Mbwana Puga mbele ya Jaji Mtema, amewaacha wenzake wanaendelea yeye amefika kwenye kesi hiyo kwa kuonesha uzito.

Hata hivyo, alidai wanashahidi mmoja na wapo tayari kuendelea kusikilizwa kwa kesi kwa sababu washtakiwa wote wawili wapo mahakamani.

Hakimu Lyamuya akawauliza washtakiwa kama wamemsikia Wakili Ngukah na kumuelewa?, mshtakiwa Nathwan alidai kuwa amesikia na amemuelewa vizuri kwamba mawakili wanapokuja wanatakiwa waje na vielelezo kuonesha walikuwepo Mahakama Kuu.

“Sikiliza nikwambie mawakili wako walipaswa kuyajua haya yote na sio kwamba hawajui wanajua vizuri kwa sababu ni wakongwe kwenye sheria kama hawapo mahakamani wanatakiwa walete taarifa wasipoleta ni kama waganga wa kienyeji.

“Wanatakiwa wafuate sheria wafuate utaratibu, kwa hiyo wanatakiwa walete vielelezo leo hawapo (jana) siku ya kesi wavilete kuonesha kamba walikuwepo huko,”alisema Hakimu Lyamuya

Hata hivyo, Wakili Ngukah aliiomba Mahakama kwamba siku nyingine likitokeq suala kama hilo basi kesi iendelee kusikilizwa bila kuwepo kwa mawakili, lengo ni kumaliza kesi hiyo.

Kesi imeahirishwa hadi Desemba 10,2024 saa sita mchana kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Wanandoa hao ambao ni raia wa Tanzania wenye asili ya India wanaoishi Mtaa wa Mrima-Kisutu, jengo la Lohana jijini Dar es Salaam wanaotuhumiwa kwa mashtaka manne waliyoyatenda Julai 21,2023 kinyume cha sheria.

Ilidaiwa kuwa Nathwan anatuhumiwa Julai 21,2023 akiwa eneo la mtaa wa Mrima-Kisutu, jengo la Lohana, ndani ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam kinyume cha sheria alimsababishia madhara makubwa Kiran Lalit kwa kuzamisha kichwa chake kwenye ndoo ya saruji iliyochanganywa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news