DAR-Siku ya maziko ya bondia Hassan Mgaya imesogezwa mbele ambapo hatozikwa siku ya leo bali atazikwa Jumatano ya Januari Mosi, mwaka 2025.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Mweka Hazina wa Chama cha Mabondia nchini Tanzania, Cosmas Cheka, imekuja baada ya baba yake kuomba mtoto wake asizikwe hadi atakaporudi kutoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ili aweze kumzika mtoto wake.
"Habari za asubuhi wadau wa ngumi napenda kutoa taarifa ya mazishi ya bondia Hassan Mgaya, kilichotokea jana Hospitali ya Mwananyamala mazishi yake yatafanyika Jumatano mzee wake ameomba mpaka yeye atakaporudi kutoka DR Congo,'' ilisema taarifa hiyo ya Cheka.
Mgaya alipoteza maisha siku ya Jumapili ya Desemba 29, mwaka huu katika Hospitali ya Mwananyamala kufuatia kupigwa kwa TKO na mpinzani wake Paulo Elias katika pambano lake lililofanyika usiku wa Desemba 29, 2024 kwenye ukumbi wa Dunia ndogo uliopo Tandale kwa Mtogole.