DAR-Naibu wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe Hamis Mwinjuma, amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Chama cha Kriketi Tanzania, Dkt. B.S. Sree Kumar, ambapo wamejadili kuendeleza mchezo huo shuleni.
Kikao hicho kimefanyika Desemba 28, 2024 katika ofisi za Wizara zilizopo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambapo wamejadili mpango wa Chama cha Kriketi Tanzania kujenga viwanja katika shule pamoja na kufanya mafunzo ya walimu wa mchezo wa Kriketi.
Dkt. Kumar amewasilisha ombi kwa Mhe. Naibu Waziri Mwinjuma kuwa, mchezo wa Kriketi uwe miongoni mwa michezo itakayochezwa kwenye mashindano ya UMISSETA mwaka 2025.
Mhe. Naibu Waziri ameahidi kulifanyia kazi ombi hilo na Wizara itafanya mawasiliano na Ofisi ya Rais TAMISEMI ili kuona uwezekano wa mchezo huo kuongezwa kwenye michezo ya UMISSETA.