Mchungaji Imani Oscar Katana ataja mambo manne ya kufanya tunapomaliza mwaka 2024 kuingia 2025

DAR-Mchungaji Kiongozi wa Moto Ulao Online Church (MUOC), Imani Oscar Katana ametaja mambo manne ambayo kila mtu anapaswa kuyafanya tunapomaliza mwaka 2024.
Mchungaji Katana ametaka shukrani zitolewe kwa Mungu kwa yote aliyotutendea katika mwaka huu yakiwemo afya, chakula, mavazi, malazi, amani na mambo mambo mengi mema; na kwa watu.

Pia,ametaka kila mmoja kwa nafasi na wakati wake kushukuru “watu waliosimama nawe, waliokubariki, na waliokuinua.”

“Mwishoni mwa mwaka ndio wakati wa kuwakumbuka wale wote waliogusa maisha yako kwa namna moja ama nyingine. Hapa unaweza kutoa sadaka au kutoa zawadi kwa watu hao muhimu,” amesema Mchungaji Katana ambaye pia anaongoza Kanisa la Kibaptist la Moto Ulao lililopo Dege, Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Katika salamu zake, Mchungaji Katana ametumia vifungu mbalimbali vya Biblia vikiwemo Yeremia 30:19 na Wakolosai 3:15.

Katika Yeremia neno linasema, “Tena kwao itasikiwa shukrani, na sauti yao wachangamkao; nami nitawazidisha, wala hawatakuwa wachache; tena nitawatukuza, wala hawatakuwa wanyonge.”

Mchungaji Katana ametaja jambo la pili la kufanya kuwa ni kupata muda binafsi wa kuutafakari mwaka 2024. “Ni muhimu kujitenga kwa muda na kutafakari maisha yako, yalivyokwenda 2024 na kuwaza utakavyoyaboresha katika mwaka 2025,” amesema mtumishi huyo wa Mungu.

Amehimiza, kila mtu kutafuta muda mzuri wa kuwaza na kutafakari yaliyopita kwa mwaka 2024 na yanayokuja 2025.

Aidha, ametaja kupanga mipango ya mwaka 2025, kama suala la tatu la muhimu ambalo kila mtu anatakiwa alifanye.

“Neno la Mungu linatuongoza kupanga na kujiandaa. Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana (Mithali 16:1),” amesema Mch. Katana katika ujumbe wake, na kuongeza kwa ujumbe ulio katika Luka 14:28-32.

Suala la nne na la muhimu ambalo Mch. Katana amesisitiza ni kwa kila mtu kuombea mipango yake ya mwaka 2025, ambapo ameshauri kuupangilia mwaka katika maeneo manne ambayo ni kiroho, kiuchumi, kimahusiano na kiafya.

Kiroho amehimiza kila kupanga kuwa karibu na Mungu kwa kutokukosa ibada, kuwahi katika ibada, kuwa msomaji wa Neno, kuwa mwaminifu katika utoaji sadaka na kuwaleta watu wengine kwa Yesu.

Kiuchumi, Mch. Katana ametaka kuombea kuboresha kipato na kuongeza kipato kutokana na shughuli mbalimbali ambazo kila mtu anafanya ili kujiletea kipato.

Kimahusiano, ametaka maombi yalenge kuomba Mungu awezeshe kuboresha mahusiano na watu ambao wana mchango chanya katika maisha yako, na wakati huo huo akupe macho ya kuona na kuwaepuka watu ambao hawana faida kwako. 

Aidha, amehimiza umuhimu wa kuombea ili kupata nafasi ya kujifunza mambo mazuri kwa watu wengine.

Upande wa afya amehimiza kujiepusha na ulaji usiofaa, kuepuka vinywaji hatarishi na kujituma kufanya mazoezi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news