Mheshimiwa Othman aweka jiwe la msingi la Mradi wa Zipline ambao ni Rafiki wa Mazingira

ZANZIBAR-Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,Mheshimiwa Othman Masoud Othman amesema, miradi ya uhifadhi wa misitu itasaidia Serikali na jamii, kwa kiasi kikubwa kuongeza mapato kupitia utalii, na hasa kuirudisha nchi katika uzuri wake wa asili, na hatimaye kujikwamua kiuchumi.
Mheshimiwa Othman ameyasema hayo Jumamosi ya Disemba 28, 2024 akiwa Mgeni Rasmi katika Hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Mradi wa Zipline, ambao ni Rafiki wa Mazingira, ulioanzishwa na Jumuiya ya 'Zanzi Eco-Tourism', huko katika Hifadhi ya Msitu wa Masingini, Wilaya ya Magharibi A, Mkoa wa Mjini- Magharibi, Unguja.

Akifafanua kauli hiyo amesema, hizo zote ni faida na tija ambazo mradi huo unaweza kuzihamasisha, hasa kwa zama hizi ambazo Nchi, na Dunia kwa ujumla, inapambana na athari za mazingira, zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi.
"Ninawakumbusha kwamba Msitu huu kutokana na umuhimu wake wa kuhifadhi maji ambayo yanatoa huduma kwa Wakaazi wa Mji wa Zanzibar; mbali na kutoa huduma hiyo, tunaambiwa Mito yote na Chem-Chem ziliopo maeneo ya Kwanyanya, Mwanyanya, Mtoni, Amani, Welezo, Mtopepo, Mwera, Bumbwisudi na Kianga, chanzo chake ni kutoka hapa Masingini."

Hivyo, amefahamisha kuwa mbali ya kutoa huduma hizo, Msitu huo ni muhimu kwa kilimo kupitia mito hiyo pamoja na Chem-chem ambazo pia amezibainisha.

“Sehemu hii ni sawa na mapafu ambayo tunavutia hewa kwaajili ya uhai wetu”, ameendelea kusema Mheshimiwa Othman akitilia-mkazo umuhimu wa pekee wa mazingira katika mnasaba wa mradi huo."
Ameeleza kuwa, ni faraja kwa Serikali kuona kwamba Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kwa kushirikiana na Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale imeandaa Miongozo ya Uwekezaji-Rafiki na Mazingira, katika maeneo ya Misitu, ambapo tayari wawekezaji wamepatikana wa kuanza kutekeleza Miradi hiyo, katika Hifadhi mbali mbali za Misitu, hapa Zanzibar.

“Miradi ya namna hii inakwenda sambamba na Mpango wa Serikali wa Kuirithisha Zanzibar ya Kijani (Zanzibar Green Legacy Program) ambapo ikiendelea vyema, na misitu itaendelea na mazingira yatakuwa rafiki kwa jamii,”amesisitiza Mheshimiwa Othman huku akiitaka Wizara ya Kilimo, pamoja na jamii kuitunza, kwani ina umuhumu wa pekee kwa maisha ya Watu wa Visiwa hivi.

Akitoa salamu za Wizara, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili, na Mifugo, Mhe. Shamata Shaame Khamis, amesema Serikali ya Zanzibar itaendelea kuthamini Miradi hiyo ambayo ni Kivutio cha Watalii, na hasa kwamba ni sehemu muhimu ya kuongeza Pato la Nchi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Ndugu Ali Khamis, ameeleza azma ya Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki kwa Wawekezaji, ili kuwahamasisha kuja kuwekeza zaidi katika maeneo mengine ya misitu, hapa Visiwani.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Zanzi Eco-Tourism, Bw. Allan Peter Nnko, amesema awamu ya kwanza ya mradi huo, itagharimu kiasi cha Shilingi Milioni Mia Tisa (900,000,000/=), na kuongeza kwamba ni kivutio salama na rafiki kwa mazingira, na kinatarajiwa kuzalisha ajira nyingi kwa Wakaazi wa Maeneo hayo.

Hafla hiyo, ambayo ni sehemu ya Shamrashamra za Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar, yanayobeba Kaulimbiu ya 'Amani, Umoja na Mshikamano kwa Maendeleo yetu', imetanguliwa na harakati mbali mbali zikiwemo za Dua na Burudani ambazo ni pamoja na Ngoma ya Kibati, kutoka Chuo cha Mafunzo Zanzibar.
Viongozi mbalimbali wa Serikali, Vyama vya Siasa, Taasisi za Mazingira, na Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama wamehudhuria hapo wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Magharib A Unguja, Ndugu Sadifa Juma Khamis.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news