Miaka 61 ya Mapinduzi nchi ina maendeleo makubwa-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amebainisha kuwa katika miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar nchi imeshuhudia hatua kubwa ya maendeleo katika miundombinu mbalimbali ikiwemo elimu, afya, umeme, maji, barabara.
Vilevile teknolojia, madaraja na bandari katika miradi yote hii wahitimu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume ni miongoni mwa wahandisi ambao waliotoa mchango mkubwa sana kufanikisha maendeleo hayo.

Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo kwenye mahafali ya 10 ya Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume iliyopo Mbweni Mkoa wa Mjini Magharibi leo Disemba 21, 2024.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi amewasisitiza wahitimu wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Karume, kuitafsiri elimu waliyoipata kwa vitendo badala ya nadharia ili kutoa mchango wao kwa maendeleo ya nchi.

Rais Dk.Mwinyi amesema Serikali itaendelea kutambua umuhimu wa taasisi hiyo kama chachu ya maendeleo kwa kuzalisha wataalamu wenye ujuzi katika sekta mbalimbali.

Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amesema, kuanzishwa kwa Taasisi hiyo ni jitihada ya kutafsiri kwa vitendo dhamira ya elimu ya amali na ufundi na kuwapa mbinu wananchi za kujitegemea ikiwa ni hatua muhimu ya ilani ya Chama cha Afro Shirazi iliyokuwa na dira na malengo ya muda mrefu ya kuandaa rasilimali watu kwa kuitumikia nchi na kusukuma mbele maendeleo.
Hatua hiyo inakwenda sawasawa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020 - 2025 inayoweka mkazo kwa vijana kupewa elimu ya amali na ufundi ili wajitegemee badala ya kusubiri ajira chache zilizoko katika mfumo wa Serikali.
Rais Dk.Mwinyi ameeleza kuwa tangu kuanza kwa Awamu ya Nane, Serikali imeipatia taasisi hiyo, miradi mikubwa miwili ikiwemo kuwajengea uwezo Vijana Kujiajiri na Kuajirika katika Sekta ya Uchumi wa Buluu pamoja na mafunzo katika sekta ya ufundi na sayansi na teknolojia yenye viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa ambayo kumalizika kwake kutaimarisha miundombinu ya Taasisi hiyo pamoja na rasilimali watu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news