DAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, ameeleza kuwa mfumo wa malipo ya taifa nchini ni imara na thabiti, unaowezesha malipo kwa haraka na kwa gharama nafuu popote nchini na kuchangia ukusanyaji wa mapato ya taifa kwa ufanisi zaidi.
Amesema kuwa, kuwepo kwa mifumo mbalimbali ya malipo kumeongeza wigo wa huduma hii na kumwezesha kila mwananchi kuchagua mfumo unaomfaa zaidi kulingana na mahitaji yake.
Gavana Tutuba ameyasema hayo tarehe 20 Desemba 2024 wakati wa mkutano na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika ofisi za makao makuu madogo za BoT, Dar es Salaam, ambapo TRA iliipongeza BoT kwa kuwa mdau muhimu na mchagizaji wa mafanikio katika utendaji wao wa kazi.
“Mfumo mpya wa Malipo ya Papo kwa Hapo (TIPS) uliozinduliwa na Mh. Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango, mwezi Machi mwaka huu, umeleta mageuzi makubwa kwa urahisi na unafuu wa kufanya malipo kwa njia ya kielektroniki kupitia simujanja,” alisema Gavana Tutuba.
Ili kuendana na kasi ya maendeleo ya TEHAMA, Gavana wa BoT amesema, Tanzania inahamia katika kufanya malipo kwa njia ya kidijitali, na Benki Kuu ya Tanzania imejizatiti kuhakikisha mifumo hii inawezesha malipo kwa ufanisi zaidi.
"Benki Kuu inaendelea kusimamia sekta ya fedha kwa weledi mkubwa, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha usalama wa fedha kupitia mifumo ya malipo ya kidijitali na kuepusha matukio ya wizi wa fedha kupitia mitandao,” amesema Gavana na kuongeza kwamba usimamizi huo unachangia katika kuimarisha uaminifu na usalama katika sekta ya fedha.
Katika mkutano huo, TRA, iliipongeza Benki Kuu kwa kuwa mshirika mkubwa wa mafanikio ya Mamlaka hiyo.
“Mashirikiano kati ya TRA na Benki Kuu yamewezesha TRA kukusanya mapato kwa weledi zaidi, ambapo katika miezi sita ya kwanza ya mwaka huu wa fedha, TRA imefanikiwa kukusanya mapato yaliyokadiriwa kwa kiwango cha zaidi ya asilimia 41 ya makadirio yao, Mkurugenzi wa Fedha wa TRA," Bi.Dina Edward amesema katika pongezi zake kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA.
Bi. Dina Edward alisisitiza kuwa Benki Kuu imechangia sana katika mafanikio haya kwa kusimamia kwa weledi Sera ya Fedha, Mifumo ya Malipo ya Taifa, Sekta ya Fedha, na Mabenki.