ARUSHA-Mkutano wa Kikanda wa Matumizi Bora ya Nishati unaojumuisha Viongozi na Wadau mbalimbali kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umeanza kwa mafanikio ambapo katika Siku ya kwanza Wadau wameweza kuonesha teknolojia mbalimbali za matumizi bora ya nishati ikiwemo majiko na magari.
Katika siku ya kwanza ya Mkutano, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio amekagua mabanda ya Maonesho ya Wadau mbalimbali wanaoshiriki katika Mkutano huo ulioanza jijini Arusha ambao utafunguliwa rasmi kesho na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko.
Pamoja na kukagua mabanda hayo ya maonesho, Dkt. Mataragio alikagua shughuli nyingine zinazoendelea kukamilishwa kuelekea siku ya ufunguzi rasmi wa Mkutano huo.
Katika Mabanda ya Maonesho, Dkt. Mataragio alijionea vifaa mbalimbali vinavyotumia umeme kidogo ikiwemo majiko, Brenda, mashine za kusukuma maji na magari ya umeme.
Dkt.Mataragio amesema kupitia REEC 2024, Tanzania inataka kutoa ujumbe wa jinsi Tanzania inavyojikita katika jitihada za kupunguza hewa ya ukaa kwa kutumia vifaa vya nishati visivyochafua mazingira.
“Katika maonesho haya nimeona kuna majiko ya umeme yanayotumia umeme kidogo na gharama ndogo kuivisha chakula, nimeona majiko ambayo yanaweza kuivisha maharage kwa gharama ya sh.300 tu ambayo ni chini ya unit moja ya umeme wakati ukitumia mkaa utahitaji shilingi 3000 hadi 4000,”amesema Dkt.Mataragio.
Naye, Lamine Diallo, Mkuu wa Sehemu ya Maliasili kutoka Umoja wa Ulaya (EU) amesema Mkutano wa Kikanda wa Matumizi Bora ya Nishati unalenga kuhamasisha matumizi bora ya Nishati kwa nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika na kwamba EU inajivunia kushirikiana na Serikali ya Tanzania na UNDP kuwezesha kufanyika kwa Mkutano huo.
Amesema pamoja na masuala mengine, Mkutano huo unalenga kuhakikisha Mamlaka mbalimbali pamoja na kaya zinalipa kipaumbele suala la Matumizi bora ya Nishati ambalo litapelekea kuwa na utunzaji wa nishati.