ZANZIBAR-Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana,Shaib Ibrahim Mohamed amesema, kuwepo kwa Mradi wa Kilimo Tija umesaidia kutoa fursa za ajira kwa vijana.
Ameyasema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi Tunzo na Ruzuku kwa Vijana Wajasiriamali waliofanya vizuri kupitia Mradi wa Kilimo Tija huko katika Viwanja vya Maonesho ya Nanenane Kizimbani Wilaya ya Magharibi A.
Aidha,amesema mradi huo pia utasaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kupunguza idadi ya Vijana wasiokuwa na ajira nchini.
Hata hivyo amewataka Vijana hao Wajasiriamali, walipata Tunzo na ruzuku ikiwemo vifaa kuvitumia vizuri ili kuweza kufikia malengo yaliokusudiwa.
Mbali na hayo amesema lengo la mradi huo ni kuwawezesha Vijana kupata mafanikio kwa kujitolea kupitia sekta ya Kilimo cha Mbogamboga na Matunda.
Hata hivyo, ameushukuru Uongozi wa USAID kwa kushirikiana na Serikali kwa kupanga na kuusimamia mradi wa Kilimo tija na kuweza kuwa mkombozi wa kiuchumi kwa jamii.
Nae Mwakilishi kutoka Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID) nchini Tanzania,Judith Kitivo amesema shirika hilo, linaendesha Mradi wa miaka 5 ambao umefikia miaka mitatu (3) na tayari umeleta mafanikio makubwa ikiwemo kutoa ruzuku na tunzo kwa Vijana waliofanya vizuri kutoa hamasa kwa wengine.
Aidha, amesema malengo ya mradi huo ni kuwaendeleza Vijana kiuchumi kwa uingizaji wa bidhaa na ajira kupitia Shamba lenye Teknolojia za kisasa,kuongeza uzalishaji pamoja na kuondoa changamoto mbalimbali zilizopo.
Kwa upande wake Meneja wa Mradi wa Kilimo Tija,Beatria Ngombe ameishuru Serikali,TGM na Milele Foundation kwa kutekeleza mradi huo chini ya Ufadhili wa Shirika la USAID.
Amesema,shirika hilo linasaidia vijana kupata mafanikiao ya sekta ya kilimo cha mboga na matunda ili kuweza kufikia kilimo endelevu.
Aidha,amesema mradi huo umetoa mafunzo kuhusu mbinu bora ya usarifu, mbinu bora za kilimo, uhifadhi wa Mazingira na elimu ya kijinsia.
Nassour Mussa ni miongoni mwa vijana walionufaika na Mradi huo, amelishukur Shirika la USAID kupitia Mradi wa Kilimo Tija kwa kutoa Msaada huo sambamba na mashirikiano makubwa walionayo jambo ambalo limesaidia kuongeza ufanisi wa kiutendaji kwa vijana hao.