Mtanzania anunua kampuni ya Bamburi Cement nchini Kenya

MOMBASA-Edhah Abdallah ambaye ni mfanyabiashara mashuhuri nchini Tanzania kupitia kampuni yake ya Amsons Industries (K) Ltd amefanikisha ununuzi wa asilimia 96.4 ya hisa milioni 362.96 za Bamburi Cement kwa jumla ya shilingi bilioni 23.2 za Kenya (zaidi ya shilingi bilioni 424.31 za Kitanzania).
Aidha,hatua hii inafanya Amsons kuwa mmiliki mkuu wa kampuni hiyo ya saruji yenye hadhi kubwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki.

Hivi karibuni,wanahisa wa Bamburi Cement waliidhinisha uhamisho wa hisa milioni 212.73, zenye thamani ya shilingi bilioni 13.83 za Kenya sawa na shilingi bilioni 252.94 za Tanzania kwa Amsons Industries.

Vilevile,hii ilikuwa ni nyongeza kwa hisa milioni 137.06 ambazo Amsons ilikuwa imenunua hapo awali, na kufanikisha ununuzi wa jumla ya hisa kwa shilingi bilioni 22.74 za Kenya bilioni (zaidi ya shilingi bilioni 415.90 za Tanzania), kila hisa ikiwa imeuzwa kwa shilingi 65 za Kenya sawa na shilingi 1,188.81 za Kitanzania.

"Ununuzi huu ni sehemu ya mkakati wetu wa muda mrefu wa kupanua uzalishaji wa saruji maalum. Ushirikiano huu mpya unalenga kuleta manufaa kwa pande zote mbili," Amsons Group imeeleza katika taarifa yao kwa vyombo vya habari.

Hata hivyo, ununuzi huu ulikuwa na changamoto. Kwa mujibu wa ripoti ya Business Daily, Amsons ilikamilisha mkataba huu baada ya kampuni ya Savannah Cement kujiondoa kwenye zabuni yake.

Mwenyekiti wa Savannah, Benson Nduta, alikumbwa na kesi za kisheria zilizohusiana na tuhuma za udanganyifu, hali iliyosababisha kampuni yake kushindwa kuendeleza zabuni ya shilingi 75 za Kenya sawa na shilingi 1,371.70 za Kitanzania kwa kila hisa.

Mamlaka ya Masoko ya Mitaji (CMA) ya Kenya ilitoa idhini rasmi ya mauzo haya, ikisisitiza kuwa wanahisa waliopinga uamuzi huo wataendelea kumiliki hisa zao ndani ya Bamburi Cement.

Kwa mujibu wa sheria za masoko ya mitaji, CMA ilieleza kuwa mchakato wa Savannah Cement ulipungukiwa na sifa stahiki baada ya mwenyekiti wake kukabiliwa na changamoto za kisheria.

Tangazo la Amsons Group kuhusu nia yao ya kumiliki asilimia 100 ya hisa za Holcim ndani ya Bamburi Cement lilichochea ongezeko kubwa la thamani ya hisa za kampuni hiyo.

Julai, hisa za Bamburi zilipanda kwa asilimia 28.33 katika Soko la Hisa la Nairobi (NSE), zikifunga biashara kwa KSh 57.75 (TZS 1056.21) kutoka KSh 49.60 (TZS 907.15) asubuhi ya siku hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news