PWANI-Mkazi wa Kibaha mkoani Pwani, Godfrey Killu anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za kumuua mke wake.
Hayo yamebainishwa leo Desemba 5,2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase wakati akizungumza na wanahabari ofisini kwake Kibaha.
Killu anatuhumiwa kwa kumuuwa mkewe aitwaye Elizabeth Sindakika ambapo tukio hilo linadaiwa kutokea usiku wa Desemba 1,2024.
Ni baada ya Godfrey Killu na mke wake huyo kwenda katika baa kwa ajili ya kunywa pombe.
Amesema kuwa, wakati walipokuwa katika baa, Godfrey alimtaka mkewe warejee nyumbani, lakini Elizabeth alikataa hali ambayo ilisababisha ugomvi ambapo Godfrey alianza kumshambulia mkewe kwa fimbo.
Kamanda huyo amesema,baada ya kumshambulia, Godfrey aliona mkewe akizirai na kumkimbiza Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani iliyopo Tumbi kwa matibabu.
"Hata hivyo, alithibitika kufariki dunia baada ya kupatiwa huduma za kwanza."
Amesema,muuguzi wa zamu aligundua kuwa marehemu alikuwa ameshambuliwa kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na alichukua hatua ya kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ambao walifika hospitalini na kumkamata Godfrey.
Kamanda huyo amesema, mtuhumumiwa huyo kwa sasa anahojiwa na mwili wa marehemu unaendelea kufanyiwa uchunguzi na utakabidhiwa kwa familia kwa taratibu za maziko.
“Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.”