NA DIRAMAKINI
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali,Hamza Johari leo Desemba 15,2024 ameshuhudia Simba Sports Club ikitembeza kichapo cha mabao 2-1 kwa CS Sfaxien kutoka nchini Tunisia.
Mheshimiwa Johari katika mtanange huo ambao umepigwa katika dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam alikuwa mgeni rasmi.
Ni kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof.Palamagamba Kabudi ambapo awali alisema ana matumiani makubwa ya Simba SC kushinda mchezo huo na kuitangaza vema Tanzania katika ulimwengu wa soka.
Katika mtanange huo mabao ya Simba yamefungwa na Kibu Dennis dakika ya 7 na la mwisho dakika ya lala salama 90' huku wageni wao wakipata bao kupitia kwa Hazem Hasen dakika ya 3.
Katika hatua nyingine,Mwanasheria Mkuu wa Serikali amekabidhi uongozi wa Simba SC shilingi milioni 10 ikiwa ni sehemu ya hamasa ya Goli la Mama kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan.