ARUSHA-Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga, amesema umeme ni ajenda kubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita inayolenga kufikisha umeme kwenye maeneo yote ikiwemo vijiji na vitongoji.
Amesema Serikali ipo kazini kuhakikisha ajenda hiyo inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa kupitia miradi mbalimbali ya umeme.
Kapinga ameyaeleza hayo wakati alipotembelea Vitongoji vya Migwala na Oloodo Larkaria kata ya Sepeko wilayani Monduli mkoani Arusha tarehe 03 Disemba 2024.
Kapinga amewatoa wasiwasi wananchi kuhusu umeme kufika kwenye maeneo ambayo bado hayana umeme akisema kuwa ili umeme ufike kwenye vitongoji ni lazima kwanza ufike kwenye vijiji vyote, ambapo vimesalia vijiji visivyozidi 70 nchini ili kukamilisha adhma ya Serikali kuhakikisha kila kijiji kinafikiwa na umeme.
Aidha Naibu Waziri Kapinga amesema tayari vijiji vyote 368 vilivyopo katika mkoa wa Arusha vimepata umeme na vitongoji 981kati ya 1656 vimefikiwa na huduma hiyo.
Akiwa kitongoji cha Oloodo Larkaria Kapinga ameeleza kuwa, Serikali imejidhatiti kufikisha huduma ya umeme kwa wananchi na kwamba viongozi wa Wizara ya Nishati wakiwa ni wawakilishi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan watahakikisha wanasimania rasilimali fedha zinazotolewa ili zitumike kama zilivyokusudiwa kufikisha umeme kwa wananchi.
Akiwa Kitongoji cha Lindikinya na Larkaria Kapinga amesema Mkandarasi amekwisha patikana na yupo katika hatua ya manunuzi hivyo hivi karibuni ataanza utekelezaji wa mradi wa umeme pamoja na kuwahakikisha wananchi kuwa Serikali itaendelea kupeleka miradi ya maendeleo ya ili kuchagiza shughuli za kiuchumi na kijamii.
Amesema mara baada ya miradi ya umeme kukamilika wananchi wataongeza shughuli za uzalishaji pamoja na kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia hasa majiko ya umeme kwani hutumia unit kidogo ambapo ametoa hamasa kwa wakazi wa eneo hilo mara baada yakupata umeme wajikite katika matumizi ya majiko hayo.
Akiwa katika Shule ya Msingi, Lukas Muhina kijiji cha Losurwa kata ya Esilalei , Kapinga amesema kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko amemwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO kutenga fedha kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili yakufikisha umeme katika shule hiyo huku matarajio yakiwa ni kunufaisha shule hiyo pamoja na maeneo jirani.
Kapinga amempongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye katika kipindi cha uongozi wake alikuta vijiji 4071 havina umeme lakini hadi hivi sasa vimesalia vijiji 70 tu ambavyo havijapata umeme.
Wilaya ya Monduli ina jumla ya kata 20 vijiji 62 na vitongoji 236. Vijiji vyote vimefikiwa na umeme sawa na asilimia 100, vitongoji 72 sawa na asilimia 30.5 vina umeme na miradi inayoendelea sasa itapelekea upatikanaji wa umeme kufikia asilimia 36.86 ya vitongoji vyote vya jimbo la Monduli.