NA DIRAMAKINI
MAKAMU wa Rais wa Chama Tawala nchini Namibia cha SWAPO, Netumbo Nandi-Ndaitwah amechaguliwa kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Namibia akiwa ni mwanamke wa kwanza kuongoza nafasi hiyo nchini humo.
Netumbo mwenye umri wa miaka 72 ameshinda kwa kura 638,560 akifuatiwa na mgombea wa Independent Patriots for Change (IPC),Panduleni Itula mwenye kura 284,186.
Matokeo hayo yametangazwa jioni ya Desemba 3,2024 na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Namibia (Electoral Commission of Namibia-ECN),Elsie Nghikembua.
“Katika uchaguzi wa urais, wagombea 15 walishiriki.Kwa mamlaka niliyopewa, mimi Mwenyekiti wa ECN, nimamtangaza
Nandi-Ndaitwah kuwa Rais Mteule wa Namibia,”Nghikembua amesema.
Hata hivyo,viongozi wa upinzani wamegomea matokeo hayo wakati yakitangazwa isipokuwa kiongozi wa Affirmative Repositioning, Job Amupanda.
Aidha, wapinzani wamepanga kwenda kuyapinga matokeo hayo mahakamani kwa madai kuwa uchaguzi haukuwa wa wazi na mambo mengine ambayo watayawasilisha.