ARUSHA-Wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro Mkoani Arusha wameitikia wito wa kutumia Nishati Safi ya Kupikia ikiwa ni hatua ya kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kulinda afya na kutunza mazingira.

Hayo yamedhihirika Desemba 8,2024 Wilayani Ngorongoro wakati wa utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa majiko ya gesi yanayotolewa kwa bei ya ruzuku ya 50% na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa ushirikiano na Kampuni ya Lake Gas wilayani humo.

Wananchi wilayani humo kwa nyakati tofauti walishukuru kwa kufikiwa na mradi na waliahidi kuwa mabalozi kwa wananchi wengine ambao hawakupata fursa ya kufika kupata huduma.

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unatekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 ambao ulizinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mwezi Mei mwaka huu.