DAR-Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeendelea kuimarisha ushirikiano wake na Shirika la Nyumba la Zanzibar (ZHC) kupitia ziara ya kikazi iliyofanywa na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) katika miradi mbalimbali ya makazi na biashara inayotekelezwa na NHC.
Ziara hiyo inalenga kubadilishana uzoefu, mbinu bora za utekelezaji wa miradi, na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika sekta ya ardhi na nyumba.
Ujumbe wa SMZ uliongozwa na Dk. Netho Ndilito, Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, akifuatana na viongozi wa ZHC na maafisa wengine.
Ziara hiyo imewafikisha katika miradi mikubwa inayotekelezwa na NHC, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano yaliyosainiwa miaka mitatu iliyopita baina ya Serikali ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Miradi Iliyoangaziwa
Katika ziara hiyo, ujumbe wa Zanzibar ulitembelea miradi ya mfano ikiwemo Samia Housing Scheme, mradi unaolenga kujenga nyumba 5,000, ambapo tayari nyumba 560 zimekamilika na kuuzwa kwa wananchi.
Aidha, walishuhudia maendeleo ya Kawe 711, mradi mkubwa wa biashara na makazi unaotarajiwa kukamilika ifikapo Februari 2026. Ziara ilihitimishwa katika Morocco Square, mradi wa kisasa unaojumuisha majengo manne yaliyojengwa kwa msingi mmoja, kwa gharama ya shilingi bilioni 137.
Akizungumzia ziara hiyo, Dk. Ndilito aliipongeza NHC kwa mafanikio makubwa katika utekelezaji wa miradi ya makazi na biashara.
“Tumeshuhudia kazi nzuri na ubunifu mkubwa unaofanywa na NHC. Ni uzoefu muhimu ambao wenzetu wa Zanzibar watautumia kuimarisha miradi yao ya makazi,” alisema Dkt.Ndilito.
Kwa upande wake, Makame Salum Ally, Mkurugenzi wa Sera na Utafiti kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makaazi Zanzibar, alitoa shukrani kwa NHC kwa kuwapa fursa ya kujifunza mbinu za kisasa za utekelezaji wa miradi, upatikanaji wa fedha, na usimamizi wa rasilimali.
“Tumejifunza njia bora za kutekeleza miradi ya makazi kwa ufanisi, ambazo tutaenda kuzitumia Zanzibar ili kuimarisha sekta yetu,” alisema Makame.