NA GODFREY NNKO
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),Dk.Irene Isaka amesema, katika kipindi cha karibuni mfuko huo umeokoa shilingi bilioni 18 kutokana na kuzuia mianya ya udanganyifu uliokuwa unafanywa na baadhi ya wanachama nchini.
"Kwa hiyo tumejitahidi kwenye hilo, kulitekeleza, lakini vilevile masuala ya udanganyifu tumejitahidi kwenye kuanza kufanya verification na zoezi la kwanza limetusaidia kuokoa shilingi bilioni 18 za wale ambao wanafanya udanganyifu."
Dk.Irene Isaka ameyasema hayo Desemba 5,2024 jijini Dodoma wakati wa kikao kazi kilichoandaliwa na mfuko huo kwa wahariri mbalimbali wa vyombo vya habari nchini.
Amesema,udanganyifu huo ulikuwa unafanyika katika maeneo mawili ikiwemo eneo la moral hazard.
"Kwamba unaenda kwa Daktari labda unaumwa malaria, lakini Daktari anapima UTI, anakuambia ufanye x-ray kitu ambacho si sahihi.
"Au moral hazard wakati mwingine unapimwa unakutwa una malaria, lakini unaandikiwa mavitamin."
Jambo lingine amesema ni matumizi mabaya ya kadi ya bima ya afya katika vituo vya afya.
"Tumekutana na matukio mtoto ameenda kufanyiwa tohara, lakini kalazwa kwa siku tatu,wakati ni huduma anaipata kwa saa chache, ila kwa sababu ni bima basi analazwa."
Amesema, ujio wa matumizi ya mfumo wa kidijitali utawawezesha kukabiliana na changamoto ya udanganyifu kwani ni thabiti na imara.
Pia, amesema hatua zilizochukuliwa, kadi 12,685 zilifungiwa kutokana na udanganyifu, mikataba 11 ya watoa huduma imesitishwa na hivyo kufanya jumla ya mikataba 55 iliyositishwa tangu mwaka 2018 nchini.
Vilevile watumishi watatu wa mfuko huo wamechukuliwa hatua za kinidhamu baada ya mashauri yao kukamilika na wengine wanane taratibu zinaendelea na hivyo kufanya jumla ya watumishi 11 waliochukuliwa hatua za kinidhamu.
Wakati huo huo amesema watumishi wa sekta ya afya wapatao 36 taarifa zao zimewasilishwa katika mamlaka za kinidhamu.
Kuhusu uhai wa mfuko, Dkt.Irene Kisaka amesema uhai wa mfuko mwaka 2001/02 ulikuwa miaka saba na miezi tisa, lakini ukashuka hadi miezi sita Juni mwaka 2023 na ulipanda hadi mwaka mmoja Juni 2024.
Pia,amesema makusanyo hadi Juni 2024 ni shilingi bilioni 756.48 sawa na asilimia 101.3 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 746.76.
Dkt.Kisaka amesema, asilimia 26.4 ya wananchi wanaishi chini ya mstari wa umaskini. Kati yao, asilimia 70 wako vijijini, wote wanastahili kupewa bima bila kuchangia popote walipo.
Aidha,amesema kuna ongezeko kubwa la wazee wa kuanzia umri wa miaka 60 ambao wana changamoto kubwa za afya, hasa magonjwa yasiyoambukiza (non-communicable disease).
Mbali na hayo, Dkt.Kisaka amesema, vituo vya kutolea huduma za afya vyenye mkataba na mfuko huo asilimia 73 ni vya Serikali, asilimia 18 ni vya sekta binafsi na taasisi za dini ni asilimia tisa.
Pia, amesema kwa kipindi cha kuishia Juni 2024 mfuko umelipa madai ya vituo vya kutolea huduma ya shilingi bilioni 650.4 ikiwa ni asilimia 37 vya Serikali, asilimia 35 kwa votio binafsi na asilimia 28 ya vituo vya madhehebu ya dini nchini.
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ni taasisi ya umma iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria Sura 395 na kuanza utekelezaji wake mwezi Julai,2001.
Lengo la kuanzishwa kwake ni kusimamia upatikanaji wa huduma bora za matibabu kupitia utaratibu wa bima ya afya ya jamii kwa wananchi ikiwemo watumishi wa umma, wategemezi wao pamoja na makundi mengine wanaojiunga kwa hiari kutoka katika sekta rasmi na isiyo rasmi.