Ninaamini Mawakili wa Serikali ni Jeshi ambalo linalinda uchumi wa nchi kwa kutumia kalamu-Wakili Mkuu wa Serikali

DODOMA-Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari ametoa wito kwa Wakurugenzi wa Divisheni/Idara na Wakuu wa Vitengo vya Sheria Serikalini kuhudhuria kwa wingi kikao kazi cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kitakachofanyika tarehe 06 Desemba, 2024 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji ulioko Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameyasema hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari tarehe 05 Desemba, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mtumba, Jijini Dodoma, ambapo alisema katika kikao hicho Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mhe. Prof. Palamagamba John Aidan Mwaluko Kabudi (Mb.),Waziri wa Katiba na Sheria.

Aidha Mhe.Johari amesema kuwa, kikao hicho kitatumika kuzikumbusha Wizara, Taasisi, Idara, Vitengo pamoja na Mawakili wa Serikali wanazotekeleza majukumu ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu masuala ya kiutendaji katika utoaji wa huduma za Sheria Serikalini.

“Nachukua nafasi hii kuwakaribisha na kuwahamasisha Wakurugenzi wa Divisheni/Idara na Wakuu wa Vitengo vya huduma za Sheria Serikalini waweze kuhudhuria kwa wingi kwenye kikao hiki muhimu,"amesema Mhe. Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Vilevile, Mhe. Mwanasheria Mkuu alisema kuwa pamoja na mambo mengine, kikao hicho kitatumika kuwakumbusha Wakurugenzi wa Divisheni/Idara na Wakuu wa Vitengo vya Sheria Serikalini umuhimu wa kuzingatia sheria, taratibu, mipango ya maendeleo, dira na miongozo mbalimbali ya Serikali inayopaswa kuizingatiwa wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Akizungumzia masuala yatakayozingatiwa zaidi katika kikao hicho aliyataja kuwa ni pamoja na, Taarifa za Utekelezaji wa kazi za Mawakili wa Serikali, ushirikiano na umoja baina ya Mawakili wa Serikali, changamoto zinazowakabili Mawakili wa Serikali, Maadili kwa Mawakili wa Serikali, Utekelezaji wa Miongozo inayotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na umuhimu wa ushirikishwaji wa Mawakili wa Serikali katika mambo yanayohitaji ushauri wa kisheria.
“Nitatumia kikao hicho kueleza dira yangu kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali itakayoharakisha kutimiza yale ambayo tumeyapanga katika mpango mkakati wetu wa mwaka 2021, 2024/25 ikiwemo kutimiza ile azima ya Weledi na Ubora”. Amesema Mhe. Johari.

Katika hatua nyingine Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa ana matumaini makubwa kuwa, kikao hicho kitazaa matunda na kutoa uelekeo na mikakati kabambe ya kutoa huduma bora za kisheria kwa Wananchi.
“Ninaamini Mawakili wa Serikali ni Jeshi ambalo linalinda uchumi wa nchi kwa kutumia kalamu,"amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika kikao hicho na Waandishi Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitoa wito kwa Wakurugenzi wa Divisheni/Idara na Wakuu wa Vitengo vya Sheria Serikalini kufika kwa wingi bila kukosa kwani kitajadili masuala mbalimbali yenye nia ya kuboresha Sekta ya Sheria Nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news