DAR-Ofisi ya Msajili wa Hazina imevuka kwa asilimia 13 lengo la kukusanya mapato yasiyo ya kodi kwa mwezi Novemba mwaka huu.
Hayo yamesemwa leo Desemba 4,2024 jijini Dar es Salaam na Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu.
“Hadi kufikia Novemba 29 tulikuwa tumekusanya Sh33.1 bilioni kama mapato yasiyo ya kodi, sawa na asilimia 113 ya lengo la kukusanya Sh29.4 bilioni kwa mwezi huo.” Bw. Nehemiah Mchechu, Msajili wa Hazina.
Mapato hayo hukusanywa kutoka kwa Mashirika na taasisi za Umma, wakala wa serikali na kampuni ambazo serikali ina hisa chache.
Vyanzo vikuu vya mapato yasiyo ya kodi ya Ofisi ya Msajili wa Hazina ni gawio, mchango kwenye mfuko mkuu wa serikali, ulipaji riba na mikopo, masafa ya mawasiliano, pamoja na ziada na michango mingineyo.